Watu kadhaa wanaswa kuhusu ukataji wa miti
Na BARNABAS BII
TAASISI ya Huduma za Misitu (KFS) Jumapili ilinasa watu kadhaa waliopatikana wakikata miti kiharamu katika Msitu wa Embobut katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Msitu huo ndio chanzo cha maji ya Cherangany.
“Washukiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuharibu msitu wa umma,” akasema Bw Dedan Nderitu, Mkuu wa Uhifadhi wa Misitu katika KFS katika ukanda wa North Rift.
Miongoni mwa shehena zilizonaswa ni miti 320 iliyokatwa katika msitu wa Tendelwa, Marakwet Mashariki ambapo kundi la wavamizi waliteketeza afisi ya KFS mwaka jana.
“Maafisa wa kulinda misitu waliokuwa likizoni wameagizwa kurejea kazini ili kuhakikisha kuwa marufuku ya siku 90 dhidi ya ukataji miti kiharamu inafaulu,” akasema Bw Nderitu.
Kulingana na KFS, ekari 25,000 za misitu ya umma zimenyakuliwa na kujengwa nyumba za makazi na taasisi za elimu.
“Wanyakuzi hao wamekuwa changamoto kubwa kwetu katika juhudi za kuhakikisha misitu inalindwa dhidi ya wakataji haramu wa miti,” akasema Bw Nderitu. Alisema Kaunti ya Elgeyo-Marakwet inaongoza kwa idadi ya makazi, shule na hospitali zilizojengwa katika misitu ya umma.
Utafiti uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara wa mbao katika eneo hilo wamesitisha shughuli zao kufuatia marufuku ya ukataji miti iliyotolewa na Naibu Rais William Ruto. KFS ilikusanya jumla ya Sh663 milioni kutoka kwa wafanyabiashara walioidhinishwa kukata miti mwaka jana.
Bw Nderitu alisema zaidi ya miche 25 itapandwa katika kipande cha ardhi cha ekari milioni 25 mwaka huu.
Ekari 1,200 zitapandwa miti katika kila Kaunti ya Uasin Gishu, 1,000, Trans Nzoia na Elgeyo Marakwet.