Idara yatabiri kupungua kwa mvua kuanzia Jumatano
Na VALENTINE OBARA
MVUA kubwa ambayo imekuwa ikinyesha tangu mwishoni mwa wiki iliyopita itaanza kupungua Jumatano katika maeneo mengi nchini, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imesema.
Mvua hiyo ambayo kufikia Jumanne ilikuwa imesababisha mafuriko na vifo vya watu na mifugo na pia uharibifu wa mali ilikuwa ni ya muda kabla msimu wa mvua ya masika uanze kati ya mwishoni mwa mwezi huu na mapema Aprili.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa jana ilitoa utabiri wake kuhusu jinsi hali itakavyokuwa kuanzia leo hadi Jumatatu wiki ijayo.
Katika nyanda za juu za maeneo ya Kati ikiwemo Kaunti ya Nairobi, kutakuwa na vipindi vya jua katika kipindi hicho. Maeneo mengine ya sehemu hii ni kaunti za Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi.
Hali tofauti imetabiriwa katika ukanda wa Pwani kwani kutakuwa na mvua katika maeneo machache leo asubuhi hasa Kusini mwa Pwani, lakini vipindi vya jua vinatarajiwa siku nzima kuanzia kesho hadi Jumapili.
Kaunti zinazopakana na Ziwa Victoria, zilizo magharibi mwa nchi na zile za maeneo ya Rift Valley pia zitashuhudia jua asubuhi kuanzia leo hadi Jumatatu ingawa maeneo machache yatapokea mvua leo mchana.
Mvua itakayonyesha mchana leo katika eneo la South Rift, hasa Kaunti ya Narok, itakuwa kubwa kuliko maeneo mengine ya Rift Valley ambapo kutanyesha, kulingana na idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini.
Kaunti za Kaskazini Magharibi mwa nchi ambazo ni Turkana, Pokot Magharibi na Samburu zimetabiriwa kuwa na jua isipokuwa katika maeneo machache lao na kesho.
Katika Kaunti za Kitui, Makueni, Machakos na Taita Taveta zilizo nyanda za chini za Kusini Mashariki mwa nchi, inatarajiwa kutakuwa na mvua asubuhi na mchana leo, ingawa jua litachomoza kesho hadi Jumatatu.
Hali sawa na hii imetabiriwa kuwepo katika Kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo zilizo Kaskazini Mashariki mwa Kenya.