Michezo

Salah atatwaa Ballon d'Or iwapo atashinda Afcon – Mourinho

June 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

 

NA CECIL ODONGO

KOCHA wa zamani wa Manchester United Jose Mourinho ameonyesha imani yake kwamba Mohamed Salah huenda akashinda taji la hadhi la Ballon d’Or iwapo tu atatwaa Kombe la Mataifa Bingwa Barani Afrika (AFCON) itakayoandaliwa mwezi Juni nchini Misri.

Salah amekuwa sehemu ya kikosi cha Mkufunzi Jurgen Klopp wa Liverpool kwa misimu miwili iliyopita huku akitwaa kiatu cha dhahabu mara mbili na kuorodheshwa mchezaji bora wa msimu wa 2017-2018.

Mwanadimba huyo mnamo Juni 8, alifunga mkwaju wa penalty kuisadia Liverpool kushinda taji la Klabu Bingwa Barani Ulaya(UEFA) kwa mara ya sita. Divorck Origi alifunga bao jingine na kusaidia Liverpool kushinda Tottenham Hot Spurs mabao 2-1 kwenye fainali hiyo iliyosakatwa nchini Uhispania.

Washambulizi Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wamekuwa wakipokezana taji la Ballon d’Or tangu mwaka wa 2008 na ni Luka Modrick aliyetamatisha mkondo huo wa mambo kwa kulishinda mwaka wa 2018.

Ingawa hivyo, Morinho anaamini kwamba mshindi huyo mara mbili wa tuzo ya mchezaji bora Barani Afrika ana talanta tu kama Messi na Ronaldo lakini atashinda Ballon d’Or tu iwapo timu ya taifa ya Misri itashinda makala ya Afcon mwaka wa 2019.

“Salah lazima ashinde Kombe la Mataifa Bingwa Barani Afrika. Kwa kuwa kipute hicho kinaandaliwa nchini mwake anatarajiwa kutambisha timu ya taifa ili kutwaa taji hilo,” akasema Mourinho.

Misri inayonolewa na kocha Javier Aguirre ipo katika Kundi A pamoja na Zimbabwe, DR Congo na Uganda. The Pharaohs itashiriki mechi ya ufunguzi wa kipute hicho kwa kuvaana na Zimbabwe mnamo Juni 21 mjini Cairo.