Habari Mseto

Naanza na makatibu wa wizara niliowalea kusaka maendeleo – Kimemia

June 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Nyandarua Francis Thuita Kimemia sasa anawataka makatibu waliopata nyadhifa zao wakati alikuwa mkuu wa utumishi wa umma wajue kuwa anawadai maendeleo mashinani katika kaunti yake.

Akiwa katika eneo la Ndaragwa amesema Jumanne kuwa atafanya juu chini kuhakikisha amesaka ufadhili wa kimaendeleo kutoka kila pembe ya dunia “nikianza na hawa makatibu ambao nimewalea.”

Alisema kuwa bajeti ya Kaunti haiwezi ikatekeleza maendeleo ya kina hasa katika maeneo kadhaa ambayo yamekuwa yametelekezwa kimaendeleo kwa muda mrefu.

“Mkiniona nimesafiri hadi Nairobi nikiandamana na baadhi ya mawaziri na madiwani wangu, sio eti tumeenda kula raha. Huwa tunaenda kuwasakama hawa makatibu wa wizara kwa kuwa ndio waratibu wa bajeti za kimaendeleo za serikali kuu,” akasema.

Alitaja makatibu kama Karanja Kibicho (Usalama wa Ndani) na Irungu Nyakera (Wizara ya Maji na Unyunyiziaji) sambamba na Dkt Nicholas Muraguri (Ujenzi na Miundomsingi) kama wale ambao anajua kwa uhakika wako afisini na ‘nimewalea’ wakati nikiwa mkuu wa watumishi wa umma katika utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki na pia miaka ya kwanza ya enzi ya Rais Uhuru Kenyatta.

“Ikiwa sote katika kaunti hii tutafanya kazi pamoja bila kususiana na kukatana miguu, manufaa yatakuwa kwa watu wetu wa Nyandarua,” amesema.

Malumbano

Amesikitika kwamba kwa muda viongozi wa Nyandarua wamekuwa wakilumbana kuhusu kila suala hivyo basi kuzima maendeleo kupatikana.

Akasema: “Ndiyo sababu mimi nimesema sitashauriana na wale wote ambao wanataka tuweke mipaka ya ni nani anafaa kutekeleza lipi la kimaendeleo hapa Nyandarua. Ikiwa ni maji haifai kuwa ni nani atayaleta, bora tu yanamfaa mtu wa Nyandarua. Sitapoteza wakati wangu nikilumbana na wengine wa viongozi wenu hapa eti kuna mipaka ya utekelezaji miradi. Kuna miradi ya serikali kuu na ya serikali za Kaunti.”

Amesema kuwa watu wote wa taifa hili hujumuika pamoja kudai maendeleo na hakuna wananchi wa serikali kuu na wale wa serikali za kaunti.

Katika hali hiyo, amewataka makatibu Nairobi waelewe kuwa “niko njiani kubisha milango” kuomba miradi ya kimaendeleo “na nitaanza na hao ambao nimewataja kwa sababu kwa sasa ni mimi niko kwa dhiki ya upungufu wa maendeleo Nyandarua.”