Waislamu wa Kaskazini na Pwani wagawanyika kuhusu Idd
Na MOHAMED AHMED na FARHIYA HUSSEIN
MGAWANYIKO baina ya Waislamu wa Kaskazini Mashariki na Pwani uliibuka tena baada ya maelfu ya waumini kumkaidi Kadhi Mkuu Ahmad Muhdhar, na kusherehekea Sikukuu ya Eid al-Fitr Jumanne badala ya leo Jumatano kama alivyokuwa ameshauri.
Mnamo Jumatatu jioni, Sheikh Muhdhar alitangaza kuwa mwezi ulitarajiwa kuandama jana jioni na hivyo maadhimisho ya mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan yafanyike leo Jumatano.
Lakini Kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale alitoa kauli tofauti na ya Kadhi Mkuu siku hiyo hiyo alipotangaza kuwa mwezi ulikuwa umeonekana.
“Mwezi mtukufu umeonekana maeneo ya Garissa, Wajir na nchi zingine za Waislamu.
Mwenyezi Mungu awabariki pamoja na familia zenu na amani iwe na nyinyi,” Bw Duale aliandika kwenye mtandao wa Twitter mnamo Jumatatu jioni.
Waumini kadhaa ambao walihojiwa na Taifa Leo walisema mgawanyiko ambao umekuwa ukitokea kila mwisho wa Ramadhan unaletwa na hisia kuwa cheo cha Kadhi Mkuu kimekuwa kikipewa tu mashehe kutoka Pwani.
Makadhi ambao wamehudumu miaka ya majuzi wote ni Wapwani. Hawa ni pamoja na Abdallah Kassim, Swaleh Abdallah Farsy, Nassor Nahdy na anayehudumu sasa, Sheikh Muhdhar.
Suala lingine ambalo waumini wanataja kama kiini cha mgawanyiko huu ni kuwa ofisi ya Kadhi Mkuu haina mamlaka ya kutangaza mwanzo na mwisho wa Ramadhan.
Kulingana na mafunzo ya Kiislamu, waumini wote wanafaa kuanza na kukamilisha mfungo na kusherehekea Idd baada ya mwezi kuonekana.
Pia hakuna uwazi kuhusu mahali mwezi unafaa kuonekana ili kuamua mwanzo na mwisho wa Ramadhan.
Akataza chuki
Jumanne, Sheikh Abu Qatadah kutoka Mombasa aliwarai Waislamu wasizue chuki kutokana na kutofautiana kwao kuhusu sherehe za Idd.
“Swala hili limekuwepo kwa muda mrefu na tunafaa kuheshimiana na kusonga mbele kwa pamoja,” akasema.
Jumatatu, serikali kupitia kwa Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i ilitangaza leo Jumatano kuwa likizo ya sherehe za Eid al-Fitr.
Siku ya Idd waumini wa Kiislamu huanza siku kwa kula tende na vitafunio vingine kabla ya kutoka nyumbani kwenda kuswali misikitini au viwanjani.