PARIS YAFURIKA: Wanyama na Timbe watua kambini Paris
Na CHRIS ADUNGO
KIKOSI cha Harambee Stars kinachojifua nchini Ufaransa kwa minajili ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 kimepigwa jeki na kuwasili kwa nyota Ayub Timbe na nahodha Victor Wanyama wa klabu ya Tottenham Hotspur inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Timbe ambaye kwa sasa huvalia jezi za Beijing Renhe nchini China, ni miongoni mwa mafowadi watakaotegemewa sana na kocha Sebastien Migne katika kikosi cha Stars nchini Misri baadaye mwezi huu.
Kwa pamoja na Wanyama, Timbe ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Genk nchini Ubelgiji aliungana na wenzake kambini mwa Stars hapo jana, siku moja baada ya makipa Farouk Shikhalo (Bandari FC) na Jeff Oyemba (Kariobangi Sharks) kutua pia Ufaransa.
Stars wanatazamiwa kushiriki mazoezi nchini Ufaransa kwa kipindi cha majuma mawili kabla ya kuelekea Misri kwa minajili ya kampeni za AFCON zitakazoandaliwa kati ya Juni 21 na Julai 19.
Timbe amekuwa katika fomu tangu apone baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mnamo Januari. Ushawishi wake uwanjani ulihisika zaidi kambini mwa Renhe mwishoni mwa wiki jana alipowaongoza kuwachabanga Tianjin Tianhai mabao 2-0 katika kampeni za Ligi Kuu ya China.
Tangu avalie jezi za Stars katika pigo la mabao 2-1 kutoka kwa Sierra Leone dhidi kwenye mojawapo ya mechi za Kundi F, kufuzu kwa fainali za AFCON, Timbe alipigwa marufuku ya mechi tatu kwa utovu wa nidhamu.
Hatua hiyo ilimnyima fursa ya kuwajibikia timu ya taifa katika michuano yote mingine ya kufuzu kwa fainali za AFCON.
Alipata jeraha baya la goti mnamo Desemba 2018 akichezea Renhe.
Upasuaji aliofanyiwa mnamo Januari 3 ulimweka nje katika mchuano wa mwisho wa kufuzu kwa AFCON uliowakutanisha Kenya na Ghana jijini Accra mnamo Machi.
Kuwasili kwake nchini Ufaransa kunajiri saa chache baada ya Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa kukiri kuridhishwa na maandalizi ya Stars.