• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
NDIVYO SIVYO: Mtu si mwathiriwa kabla ya kuathiriwa kwenyewe

NDIVYO SIVYO: Mtu si mwathiriwa kabla ya kuathiriwa kwenyewe

Na ENOCK NYARIKI

“HOFU imetanda eneo la Likoni jijini Mombasa kufuatia ripoti kuwa magenge ya majambazi sasa yanawadunga waathiriwa sindano za kuwafanya wapoteze fahamu kabla ya kuwaibia….”

Taarifa hii ilijitokeza katika kimojawapo cha vyombo vya habari.

Mwandishi wayo amefaulu katika kuitumia lugha sahili inayoeleweka kwa wasomaji wa kawaida ambao lengo lao ni kupashwa habari bali si kuuchokonoa usarufi wazo.

Aidha, amezingatia upatanisho wa kisarufi wa nomino ya jamii “genge”.

Aghalabu, baadhi ya waandishi hujikuta wameziingiza nomino za jamii katika ngeli ya A-WA.

Hata hivyo, makosa kadha ya athari ya lugha ya Kiingereza yanajitokeza katika kifungu hiki. Nitaliangazia kosa mojawapo.

Katika lugha ya Kiingereza, huenda neno waathiriwa ambalo fasiri yake ni “victim” likatumiwa pia kuwarejelea watu ambao wako katika hatari ya kukumbwa na matukio yanayosababisha madhara fulani.

Sivyo ilivyo katika lugha ya Kiswahili ambapo; kwanza, neno athiri kwa ujumla wake linaweza kuibua dhana ya ushawishi.

Mtu anaweza kushawishiwa kwa njia chanya au hasi.

Pili, na muhimu sana, mtu hawi “mwathiriwa” kabla ya kukumbwa na kitendo ambacho kitamfanya kujikuta katika hali hiyo.

Kabla ya kuingia katika kitovu cha mjadala, ni muhimu kufasili jina ‘mwathiriwa’.

Tumetaja kwamba kitenzi athiri kinapotumiwa kwa ujumla wake; yaani bila kufuatishwa na maneno yatakayosaidia kukiweka katika muktadha faafu, huzua utata.

Ijapokuwa kamusi imetoa maana nne za kitenzi hicho, tutaingazia maana kwa mujibu wa kifungu chetu.

Kulingana na kifungu hicho, neno waathiriwa lilidhamiriwa kuibua maana ya watu waliokumbwa na madhara. Kosa ambalo mwandishi amelifanya ni kuwarejelea watu ambao wako katika hatari ya kukumbwa na madhara kama waathiriwa.

Je, mtu huwaje mwathiriwa kabla ya kuathiriwa?

Katika lugha ya Kiswahili, maana mojawapo ya neno “mwathiriwa” ni aliyekumbwa na madhara fulani. Kwa hivyo, mwandishi wa taarifa angeitanguliza taarifa yake kwa neno “watu” kabla ya kulitumia neno waathiriwa baadaye kuwarejelea watu wenyewe.

Bora kuwaita wakazi

Na kwa sababu eneo la tukio limetajwa, basi isingekuwa hatia kuwaita watu wenyewe wakazi.

Katika sehemu, kifungu hicho kingeendelezwa hivi: “ Hofu imetanda … kufuatia ripoti kuwa magenge … sasa yanawadunga wakazi sindano za kuwafanya kupoteza fahamu kabla ya kuwaibia….”

Alhasili, mtindo wa Kiingereza wa kuandika taarifa ni tofauti na mtindo wa Kiswahili kwa sababu lugha hizo mbili huwa na fasili tofauti za msamiati wake.

Mathalani, jinsi neno mwathiriwa au “victim” linavyoeleweka katika Kiingereza ni tofauti na lugha ya Kiswahili ambapo lugha ya pili huwa na mtazamo mpana wa neno lenyewe.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Adai alitenda dhambi kuonja asali, ataka...

VITUKO: Tangazo la gavana wa benki kuu lahangaisha mgema wa...

adminleo