Mzozo wa kilabu cha Simmers: Mmiliki ataka wakurugenzi wasukumwe jela
Na RICHARD MUNGUTI
MMILIKI wa kilabu na mkahawa maarufu cha Simmers kilichobomolewa Ijumaa wiki iliyopita Bw Suleiman Murunga amewashtaki wakurugenzi wa kampuni mbili zinazozozania ploti hiyo.
Katika kesi anayoomba iratibiwe kuwa ya dharura Bw Murunga anaomba wakurugenzi wa kampuni za Nilestar Holdings na Green Valley wafungwe jela kwa kukaidi agizo la mahakama kuu na kubomoa kilabu hicho.
Bw Murunga anaomba mahakama kuu iwasukume jela miezi sita wakurugenzi wa kampuni hizi mbili kwa kuidharau mahakama.
Mbunge huyo wa zamani anasema kubomolewa kwa kilabu hicho ni njia ya kuikejeli korti na anaomba korti “iwasukume jela wakurugenzi wa makampuni hayo ndipo sheria na hadhi ya korti idumishwe.”
Pia anaomba korti iwashurutishe wakurugenzi hao wamlipe gharama na kuamuru atambuliwe kuwa mmiliki wa ardhi hiyo.
Ploti hiyo inadaiwa na Bw Madatali Ebrahim, wanawe Jalaledin Ebrahim na Jamilleh Ebrahim ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Nilestar pamoja na Bi Margaret Wairimu Magugu ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Green Valley.
Bw Murunga amewashtaki wakurugenzi hao pamoja na MabwKinyanjui Magugu, Gisbon Muchiri Ndungu na wakili Leo Masore Nyangau.
Anaomba wote wasukumwe jela kwa kukaidi agizo la mahakama kuu iliyotolewa mnamo Julai 14, 2014 na Desemba 2016 ikiwazuia wasimtatize Bw Murunga kwa njia yoyote ile.
Sh9 milioni
Waliobomoa kilabu hicho walidai kodi ya nyumba ya Sh7,560,000, ada ya wakili Sh756,000 na ada ya madalali ya Sh910,860.
Bw Murunga anasema wakurugenzi wanaodai umiliki wa jengo hilo walijua kwamba kuna maagizo ya mahakama ya kuwazuia kudai umiliki wa ardhi ambapo kilabu kimejengwa.
Mbunge huyo wa zamani anaomba mahakama ifutilie mbali maagizo mawili yaliyotolewa dhidi yake.
“Ikiwa mahakama haitaingilia mzozo huu bila shaka walalamishi wataingilia na kuanza kujenga, “anasema mlalamishi.
Wakurugenzi wa makampuni hayo yaliwasilisha kesi ya kumtimua kwenye ploti hiyo Feburuari 20 2018 mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani.
Jaji Elijah Obaga alimwamuru Bw Murunga awakabidhi wakurugenzi wa Green Valley na Nilestar nakala za kesi hiyo aliyoamuru isikizwe Aprili 4, 2018.
“Nimesoma kesi iliyowasilishwa na Bw Murunga na kutambua anaomba maagizo makuu yatolewe ya kumtambua mmiliki wa ardhi iliyojengwa kilabu hicho,” alisema Jaji Ombaga.
Miaka 32 iliyopita
Mzozo wa umiliki wa ploti hiyo ulianza miaka 32 iliyopita kati ya Bw Madatali na aliyekuwa Waziri marehemu Arthur Magugu.
Ardhi hiyo ilikuwa imeandikishwa kwa jina la Nilestar na Bw Magugu.
Ushahidi uliopo ni kwamba Bw Magugu alikuwa auziwe ploti hiyo na wenye hisa wa Nilestar kwa bei Sh25 milioni. Alilipa Sh19milioni kisha mzozo ukazuka mpango ulipotibuka.
Bw Magugu aliwasilisha kesi mahakamani mnamo 1989 na mnamo 1996 maagano mapya ya kuuzia kilabu hicho kampubi ya Green Valley na Margaret Magugu kwa $ 1.4 ukatiwa saini.
Bw Murunga hatimaye aliibuka akiwa na hati ya umiliki wa ploti hiyo.