AFCON: Senegal imani kwa kikosi cha Kombe la Dunia
Na CHRIS ADUNGO
MWISHONI mwa wiki jana, kocha Aliou Cisse wa timu ya taifa ya Senegal aliwadumisha wachezaji 16 aliowategemea kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018 katika kikosi kitakachoshiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri mwezi huu wa Juni.
Katika kikosi chake cha wachezaji 25 kinachojiandaa kwa kipute hicho, Cisse atajivunia huduma za washambuliaji waliotamba zaidi katika ligi zao mbalimbali msimu huu.
Kati yao ni Mbaye Diagne aliyefungia Galatasaray jumla ya mabao 30 katika kampeni za Ligi Kuu ya Uturuki msimu huu, Mbaye Niang aliyeibuka Mfungaji Bora wa kikosi cha Rennes nchini Ufaransa na Sadio Mane aliyetawazwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupachika wavuni magoli 22.
Miongoni mwa wachezaji ambao Cisse aliwadondosha katika orodha ya Kombe la Dunia ni beki Kara Mbodji, 29 anayetatizwa sana na jeraha la goti.
Mbodji amekuwa na kibarua kigumu msimu huu baada ya mpango wa kumtuma kambini mwa Nantes ya Ufaransa kwa mkopo kugonga mwamba.
Hatua hiyo ilimweka katika ulazima wa kurejea katika kikosi chake cha awali cha Anderlecht nchini Ubelgiji.
Aidha, alikiri kwamba ana wachezaji wengi sana ambao wana uwezo wa kulijaza pengo la Mbodji.
“Wanasoka kama vile Salif Sane (Schalke) na Kalidou Koulibaly (Napoli) wamedhihirisha kwamba wana utajiri mkubwa wa vipaji na uwezo wa kudhibiti vilivyo safu yetu ya ulinzi,” akasema Cisse.
Wachezaji wengine ambao kocha huyo anahisi kwamba wana ushawishi mkubwa katika safu ya nyuma ya Senegal ni Cheikhou Kouyate (Crystal Palace) na Pape Abdou Cissa (Olympiakos).
Cisse atemwa
Miongoni mwa wachezaji ambao kwa sasa wametemwa na Cisse licha ya kutambisha Senegal nchini Urusi mwaka 2018 ni kipa wa kikosi cha Horoya, Khadim Ndiaye anayeuguza jeraha la mguu na mvamizi Moussa Sow ambaye amestaafu soka ya kimataifa.
Wengine ni Mame Biram Diouf, Cheikh Ndoye, Adama Mbengue na fowadi wa zamani wa West Ham United, Diafra Sakho.
Nyota wapya ambao Cisse amewajumuisha katika kikosi chake kitakachochuana na Kenya, Tanzania na Algeria katika Kundi C nchini Misri ni kiungo wa zamani wa Newcastle United, Henri Saivet.
Sogora huyo ambaye kwa sasa anachezea Bursaspor nchini Uturuki hajavalia jezi za Senegal tangu Machi 2018.
Makipa: Abdoulaye Diallo (Rennes), Alfred Gomis (SPAL), Edouard Mendy (Reims).
Mabeki: Kalidou Koulibaly (Napoli), Moussa Wague (Barcelona), Pape Abdou Cisse (Olympiakos), Salif Sane (Schalke), Youssouf Sabaly (Bordeaux), Lamine Gassama (Goztepe), Saliou Ciss (Valenciennes), Cheikhou Kouyate (Crystal Palace).
Viungo: Alfred Ndiaye (Malaga), Santy Ngom (Nancy), Idrissa Gana Gueye (Everton), Keprin Diatta (Club Brugge), Badou Ndiaye (Galatasaray), Sidy Sarr (Lorient), Henri Saivet (Bursaspor, Uturuki).
Mafowadi: Ismaila Sarr (Rennes), Keita Balde (Inter Milan), Mbaye Niang (Rennes), Moussa Konate (Amiens), Mbaye Diagne (Galatasaray), Sada Thioub (Nimes), Sadio Mane (Liverpool, Uingereza).