• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WANDERI: Kisa cha Ng’ang’a ishara ya uasi wetu kwa Mungu

WANDERI: Kisa cha Ng’ang’a ishara ya uasi wetu kwa Mungu

Na WANDERI KAMAU

ALIPOANDIKA kitabu The Origin of Species (Asili ya Viumbe) mnamo 1869, lengo kuu la msomi Charles Darwin lilikuwa kujaribu kutathmini ulinganifu wa mwanadamu na viumbe wengine.

Ingawa utafiti wake ulilenga kuongeza maarifa katika nadharia kadhaa za asili ya uumba zilizopo -wanyama na mimea- Darwim alikubaliana na wananadharia waliomtangulia kwamba mwanadamu ana uwezo mkubwa wa kiakili.

Ni kauli ambayo imefikiwa na nadharia zote za uumba, kuwa kati ya viumbe wote walio duniani, upekee mkubwa alio nao mwanadamu ni uwezo mkubwa wa kiakili kuwazidi viumbe wale wengine.

Katika nadharia za kidini zilizopo, inaelezwa kuwa Mungu alimpa mwanadamu uwezo huo ili kuidhibiti dunia na kuendeleza uumba wake kwa njia ya kuzaana.

Hivyo, kauli zote zinakubaliana kuwa ukaribu wa mwanadamu na Mungu ni mkubwa sana yakini ndipo alimwacha kama “mwangalizi” wa uumba wake duniani.

Hata hivyo, kinaya kikuu ni kwamba, licha ya upekee huo wa kimaumbile na ukaribu alio nao mwanadamu na Muumba wake; amemgeuka.

Mwanadamu aliyeumbwa kwa “mfano wa Mungu” amemgeuka Mungu mwenyewe -vitendo vyake vinakinzana wazi na uwezo aliopewa na Muumba.

Amegeuka hayawani. Katili. Mdanganyifu. Mbinafsi. Muuaji na aliyejawa na tamaa.

Mwanadamu amemdhihaki Muumba aliyempa mamlaka kuudhibiti uumba wake. Ni kama mtoto aliyemgeuka mzazi aliyejitolea kwa hali na mali kumsomesha.

Ninatoa kauli hii kufuatia video iliyochipuka majuzi katika mitandao ya kijamii, ambapo ‘Mchungaji’ James Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism Centre, Nairobi, alinaswa akiwatukana maaskofu na washirika wake.

Kwenye video hiyo, ‘mchungaji’ huyo anasikika akiwataka maaskofu hao “kutii lolote analosema” bila kumuuliza maswali. Vile vile, anawaonya kuhusu “adhabu kali” kwa yeyote ambaye hatamheshimu mkewe.

Kuna fasiri nyingi ambazo zimetolewa kuhusu kisa hicho, hasa miongoni kwa viongozi na wadadisi wa masuala ya kidini.

Kwa wengi, tukio hilo ni dhihirisho la “siku za mwisho” kama ambavyo imetabiriwa katika vitabu mbalimbali vya kidini.

Hata hivyo, kauli yangu ni kuwa mwanadamu amekiuka mamlaka aliyopewa na Mungu kuudhibiti uumba wake.

Utakatifu wa dini umeingizwa kila aina ya unafiki. Mkanisa mengi ya kisasa yamegeuzwa ngome za kila aina ya maovu, kwa kisingizio cha “kuendeleza injili.”

Alipotangaza kujiondoa katika kanisa la Katoliki na kuanza kanisa la Lutheran mnamo 1793, mwanaharakati Martin Luther aliwakashifu mapapa waliokuwepo wakati huo kwa kuligeuza kanisa hilo kama “mali yao binafsi.”

Baadhi ya mapapa walilaumiwa kwa kuwa na wapenzi wa kike ambapo waliwaweka hata makanisani. Licha ya hayo, washiriki wengi wa kanisa hilo waliogopa kuwakosoa.

Lengo kuu la Luther lilikuwa kuanzisha mwamko mpya wa kidini, ambao ungewapa waumini usemi na uhuru zaidi wa kumwabudu Mungu kwa njia wazitakazo.

Hili lilidhihirisha uwezo wa kiakili katika maamuzi aliyofanya.

Janga hili litaendelea kutaasisika ikiwa watetezi wa ukweli watabaki kimya. Wanaposimama kuutetea ukweli, lazima ‘viongozi-miungu’ wa kidini wachukuliwe kama wahalifu na kukabiliwa kisheria.

[email protected]

You can share this post!

Uchafuzi wa maziwa ya Bonde la Ufa unavyoathiri utalii

NGILA: Tusirukie intaneti ya 5G, tueneze mawimbi ya 4G...

adminleo