• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
NGILA: Tusirukie intaneti ya 5G, tueneze mawimbi ya 4G kwanza

NGILA: Tusirukie intaneti ya 5G, tueneze mawimbi ya 4G kwanza

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA miezi miwili iliyopita, kumekuwa na gumzo kuhusu uwezo wa kipekee wa mtandao wa 5G ambao wadau wa teknolojia wanauona kama utakaoleta mageuzi ya kiuchumi kote duniani.

Ni kweli kwamba teknolojia hii itawazidishia wanadamu kasi ya kutuma data kupitia intaneti hadi mara mia zaidi kuliko mtandao wa sasa wa 4G. Lakini, je, Kenya iko tayari?

Kufikia sasa, kampuni tatu kuu zinazosambaza mawimbi ya 4G, Safaricom, Airtel na Telkom bado hazijafanikiwa kueneza teknolojia hiyo hadi mashinani.

Wananchi mashinani bado wanafurahia kasi na huduma za mawimbi ya 2G na 3G, kwa kuwa kampuni hizi ambazo zimekuwa zikishirikiana na serikali bado hazijaweza kuwekeza katika mitambo ya 4G katika maeneo mengi ya kaunti zote.

Unapaswa kuelewa kwamba ili mtandao wa 5G uanze kuvumishwa, lazima maeneo husika mwanzo yawe na mitambo ya 4G inayotumiwa kukweza mawimbi na kufikia kasi ya 4G.

Ningependa kueleza wazi kuwa teknolojia ya 5G itatufaa sana hasa kwa kuunganisha mabilioni ya vifaa kupitia intaneti huku huduma za kiroboti na kiotomatiki zikisaidia kupunguzia watu gharama na muda.Itakuwezesha kufuatilia na kusimamia mali yako yote kama simu, kompyuta, kamera, televisheni, benki, elimu, uwekezaji na biashara nyinginezo kupitia kwa intaneti ya moja kwa moja.

Inatazamiwa kugeuza sekta za kilimo, fedha, utalii, usalama na afya.

Hivyo, utoshelevu wa chakula, kukomesha wizi wa fedha za umma, kuzima majangili na wezi wa kimabavu huku huduma za afya zitafanikishwa kwa njia bora zaidi.

Ni mojawapo ya teknolojia ambazo shirika la Ubora wa Bidhaa nchini (Kebs) linaweza kutumia kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa feki na huduma duni.

Wenye vyeti ghushi vya chuoni pia watakuwa pabaya kwani 5G itawezesha kutambua watu hawa. Pia, Benki Kuu ya Kenya itanufaika kuzima wanaosambaza noti feki za pesa.Lakini Kenya itafikia ndoto hii lini?

Mwanzo, serikali inafaa kuzidi kushirikiana na kampuni za huduma za simu kuhakikisha mawimbi ya 4G yamefika vijijini ili sote tufurahie huduma bora za teknolojia hii.

Lazima mitambo ya 4G iwekwe mashinani na sera madhubuti kuundwa kusimamia usambazaji wa mtandao huu.Kufanya hivi kutatoa nafasi na kuunda njia ya mtandao wa 5G kuzinduliwa Kenya, jinsi ilivyofanya Afrika Kusini hapo Februari 2019.

Mafunzo pia yatakuwa nguzo muhimu kwa watu kuelewa teknolojia hizi iliwasije wakafikiria kuwa kampuni za huduma za simu zinatumia nguvu za kishetani kuleta huduma za kipekee.

[email protected]

You can share this post!

WANDERI: Kisa cha Ng’ang’a ishara ya uasi wetu kwa Mungu

MUTANU: Wazazi wasipowaelekeza watoto, upotovu utazidi

adminleo