• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
NGUGI: Viongozi wawe mfano bora maana wengi huwafuata

NGUGI: Viongozi wawe mfano bora maana wengi huwafuata

Na MWITHIGA WA NGUGI

Wavyele hawakukosea walipolonga kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, na si utani kwamba si watoto tu, bali jamii nzima kwa jumla huiga yanayotendwa na viongozi wao.

Viongozi wanaposhambuliana kwa cheche za maneno kwenye mikutano yao kadamnasi ya halaiki, matokeo yake mara nyingi huwa ni ya kupotosha kizazi cha kesho.

Kwa mfano kilichotokea kati ya Gavana wa Nairobi, Mheshimiwa Mike Sonko na Mwakilishi Mwanawake wa Nairobi, Bi Esther Passaris siku ya kuadhimisha Sikukuu ya Madaraka, ilikuwa ni fedheha tupu na jambo la kuwadhalilisha wanawake wote kwa jumla.

Kwa upande mwingine ni lazima tukumbuke kwamba uongozi sio tu uongozi na nyadhifa za kisiasa, uongozi huanzia nyumbani.

Kama kila uchao tabia za kina baba na mama ni za malumbano na matusi, vivyo hivyo watoto wao huiga wasikiayo na waonayo, wakiitana kelbu, fisi au hata mwizi; watoto hujua kwamba mtu anapokasirishwa na mwenzake, maneno kama hayo ndiyo yanayofaa kutumiwa dhidi yake, lakini kumbe haya ni matusi jamani!

Mauaji ya wachumba

Miaka ya hapo awali ilikuwa ni vigumu sana kusikia wanandoa wakifikia kiwango cha kuuana. Kwa kiwango kidogo sana palitokea talaka au labda utengano wa muda ambao familia husika zilijitwika jukumu la kuwarejesha wanandoa pamoja.

Lakini leo hii kuna shida, kila uchao tunasikia kuhusu mauaji ya wachumba wachanga hata wale ambao hawajafunga ndoa wala hata hawajaishi pamoja!

Ama kweli ibilisi ametoka kwenye maficho yake na kuanza kurandaranda kwenye miji na vitongoji vyetu pasi ufahamu wetu.

Kusema kweli ulimi ni kiungo kidogo sana, lakini ni upanga mkali kuliko panga zote.

Ewe kiongozi mwenye wadhifa unapopewa hicho kipaaza sauti na kutizama kamera za runinga, ni sharti ujue jinsi ya kuutumia ulimi huo wako, si vyema kuwakejeli viongozi wenzako hata kama ni wapinzani wako wa kiwango gani na kama ni lazima basi na hilo lifanyike faraghani kivyenu na huko hata mkitaka kuraruana basi huko mko huru.

Wa leo wazazi wanalia kuona jinsi nidhamu na tabia za watoto wao zilivyodorora lakini mengi ni yale wanayoyasoma kutoka kwa wakubwa wao.

Unalia eti wananfunzi wanaiba mitihani ili wapate alama za juu japo kwa kupitia njia za mikato, tukijisahaulisha kuwa hata kwenye chaguzi zetu hapa na pale, fununu zipo kuhusu wizi wa kura ili mwanasiasa fulani apate kiti fulani hata kama ‘hatoshi mboga’.

Hata hivyo sote hatufai kujitia hamnazo, mzigo tulionao wa kukikuza kizazi cha kesho u mabegani mwetu sisi sote kuanzia nyumbani hadi kwa wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi.

Tusisahau wazi kuwa, mti mkuu ukigwa nyuni wake huyumba; wakati wa kubadilisha mienendo ni sasa.

[email protected] 

You can share this post!

ONYANGO: Sura ya 6 ya katiba kuhusu maadili haina maana,...

Wakuu wa Oil Libya wakana kuiba Sh1.5m

adminleo