Habari Mseto

HUDUMA NAMBA: Chifu atuzwa Sh100,000 kwa kusajili watu wengi

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEORGE MUNENE

NAIBU chifu ambaye kata yake iliongoza katika usajili wa Huduma Namba katika Kaunti ya Kirinyaga ametuzwa Sh100,000.

Bw John Murikuki, ambaye ni naibu chifu wa Kata Ndogo ya Kithumbu, alipewa fedha hizo na Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP) katika kaunti hiyo, Bw Mureithi Kang’ara katika mji wa Kagio.

Kata hiyo iliwasajili watu 102,251, na hiyo ilikuwa idadi kubwa zaidi ikilinganishwa na kata zingine.

Akimpa fedha hizo, Bw Kang’ara alisema alikuwa akitimiza ahadi yake ya kumzawadi naibu chifu ambaye angewashinikiza wakazi wengi kujisajili.

“Ninatimiza ahadi yangu niliyotoa wakati shughuli hiyo ilipoanza,” akasema Bw Kang’ara.

Alimtaja naibu chifu huyo kama mwenye bidii zaidi, ambaye anapaswa kutambuliwa kwa bidii yake.

“Kama mojawapo wa maafisa wakuu wa chama tawala, nina furaha kwani Bw Muriuki aliibuka bora zaidi katika kuwashinikiza wakazi kujisajili hapa Kirinyaga,” akasema.

Aliiomba serikali ya kitaifa kutathmini uwezekano wa kumpandisha mamlaka kwa bidii yake.

Bw Muriuki aliahidi kuendelea kujitolea kuwahudumia wakazi.

Usajili huo wa Huduma Namba ulikamilika mwezi uliopita kwenye shughuli ambayo iliendeshwa kwa karibu miezi miwili.

Kwa sasa serikali inaendeleza shughuli ya kusafisha data iliyokusanywa ili kuhakikisha habari kamili za kila mtu ndizo zime kwenye sajili ya serikali.

Usajili huo mwanzoni ulikumbwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wale ambao walihofia usalama wa data yao huku wengine wakihussiha shughuli hiyo na nambari ya 666 ambayo imetajwa kwenye Biblia kama nambari ya kishetani.