• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Hatua na nadharia muhimu katika kujifunza na ufundishaji wa lugha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Hatua na nadharia muhimu katika kujifunza na ufundishaji wa lugha

Na MARY WANGARI

TUNAENDELEZA mada kuhusu mchakato wa kujifunza pamoja na kufundisha lugha ya Kiswahili.

Jinsi tulivyofafanua awali, katika shughuli hii, ni muhimu kwa mwalimu kuwapa wanafunzi fursa ya kuchunguza, kugundua, kutalii na kutafiti masuala mbalimbali kuhusu lugha ya Kiswahili.

Hatua hii ina manufaa yafuatayo kwa wanafunzi husika:

i. Itawapa wanafunzi uwezo wa kukuza lugha ya Kiswahili kila siku aweze kuongeza msamiati kwa kusoma vitabu mbalimbali vya hadithi.

ii. Watapata fursa ya kutumia mbinu mbalimbali za lugha ili kukuza uelewa wao.

iii. Wanafunzi watapata nafasi ya kukuza fikra zao na kudadisi.

iv. Itawasaidia kufanya uvumbuzi kuhusu vipengele vya mfumo na utamaduni wa lugha ya Kiswahili.

Nadharia kuu za kujifunza lugha ya pili

Katika ufundishaji wa lugha, kuna mambo mawili muhimu ambayo kila mwalimu anapaswa kufahamu. Ni muhimu kuelewa kuwa mbinu zinazohusika katika kujifunza lugha ya pili ni nyingi sawa na jinsi walimu walivyo wengi. Ni jambo la busara kutilia maanani mazingira halisi wakati wa kujifunza lugha husika.

Kwa mujibu wa Rogers (2001), wakati wa ufundishaji wa lugha ya kigeni ni muhimu kutumia mbinu mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wafikie malengo yao.

Katika shughuli ya kujifunza lugha, kuna nadharia nne kuu zinazohusika. Tutaziainisha na kuzichambua nadharia hizo jinsi ifuatavyo:

Nadharia ya hulka

Nadharia hii iliasisiwa na mwanaisimu Noam Chomsky (1957).

Hoja kuu ya mwanafalsafa huyu ni kwamba binadamu huzaliwa akiwa na uwezo kwa maana kwamba katika ubongo wake, ana mfumo ambao huzaliwa nao kwa ajili ya kujifunza lugha.

Ana kifaa kinachoitwa Language Acquisition Device (LAD) yaani Kifaa cha upataji lugha. Brown (2000), anaunga mkono mawazo haya. Mtaalam mwingine aliyeunga mkono hoja ya Chomsky ni Ellis (1997).

Watalaamu hawa walikuwa na hoja kwamba kuna kipindi mtu akifikia umri fulani hawezi kupata lugha sawasawa na wazawa wa lugha husika.

Umri huo ni kuanzia miezi 0-18.

Kwa mujibu wa wataalamu hawa mazingira hayana msaada wowote katika mtu kujifunza lugha.

 

Je, umeipenda mada hii? Tuandikie maoni au wasiliana na mwandishi: [email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publisher.

You can share this post!

LISHE: Namna ya kutengeneza sandwich

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia za kujifunza na...

adminleo