Michezo

Hekaheka za uchaguzi Leopards zashika kasi

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

MWANASOKA mstaafu, Dan Shikanda ambaye anawania kiti cha mwenyekiti katika uchaguzi ujao wa klabu ya AFC Leopards, amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa zamani wa klabu hiyo.

Hii ni baada ya tume iliyoundwa kusimamia uchaguzi huo kutangaza majina ya watu watatu watakaowania wadhifa huo.

Mbali na Shikanda, wagombeaji wengine ni Ronald Namai na Ben Musundi.

Mwenyekiti wa sasa, Dan Mule amesema hatatetea kiti hicho baada ya kukumbwa na wakati mgumu akiwa kwenye usukani.

Wengine ni Oliver Imbenzi Napali na Maurice Choge Chichi ambao watapigania kiti cha mweka hazina.

Kamati inayosimamia uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Juni 23 imesema imezima watu kadhaa kutokana na sababu mbali mbali.

Katibu wa kamati hiyo, Beron Aberi aliyeandamana na mweka hazina, Lawrence Weche alisema Katibu Mkuu wa sasa wa klabu hiyo, Oscar Igaida ni miongoni mwa waliozimwa kuwania viti kwenye uchaguzi huo.

Upendeleo

Hata hivyo, wakati mipango hiyo ikiendelea, malalamishi yamezuka kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo ambao wanapinga mikakati iliyowekwa, wakidai inapendelea watu fulani wakiwemo maafisa wa sasa wa klabu hiyo.

Majina mengine ya watu waliopigwa marufuku ni pamoja na Maurice Amahwa aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya kuokoa Leopards, mshambuliaji mstaafu, Bonface Ambani.

Kadhalika kamati ya kusimamia uchaguzi chini ya Geoffrey Serede imeondoa jina la Omboko Milemba ambaye alikuwa ameonyesha nia ya kuwani kiti cha mwenyekiti, pamoja na Richard Ekhalie.