Serikali yaonya wanaokataa noti ya sasa ya Sh1000
Na LEONARD ONYANGO
SERIKALI Alhamisi imeonya wamiliki wa nyumba wanaohangaisha wapangaji kwa kuwataka wasilipe kodi ya nyumba kwa kutumia noti ya Sh1000.
Msemaji wa Serikali Kanali (Mstaafu) Cyrus Oguna amewataka wapangaji ambao wameagizwa na wamiliki wa nyumba kutotumia noti ya Sh1000 kulipa kodi ya nyumba, kuripoti kwa polisi.
Baadhi ya notisi zinazodaiwa kuandikwa na wamiliki wa nyumba katika mitaa fulani jijini Nairobi imekuwa ikisambazwa katika mitandao ya kijamii ikiwataka wapangaji wao kutotumia noti ya Sh1000 kulipa kodi ya nyumba.
Wakati wa sherehe za Madaraka Juni 1, Gavana wa Benki Kuu Patrick Njoroge alitangaza kuwa noti ya Sh1000 inayotumika sasa itakosa kazi kuanzia Oktoba 1, mwaka huu.
Dkt Njoroge aliwataka Wakenya kurejesha noti hizo za Sh1000 katika benki wapewe noti mpya kabla ya kupoteza thamani.
“Noti ya Sh1000 bado ni halali na itakosa thamani kuanzia Oktoba 1. Watu wanaohangaishwa kwa kutumia noti ya Sh1000 waripoti kwa polisi ili wahusika wachukuliwe hatua,” akasema Bw Oguna.
Wakati huo huo, serikali imesema kuwa Wakenya wataanza kunufaika na nyumba nafuu kuanzia Septemba, mwaka huu.
Kulingana na msemaji wa serikali, nyumba 228 zinazojengwa katika mtaa wa Park Road, Nairobi zitakamilika katika kipindi cha miezi miwili na zitakabidhiwa kwa Wakenya ambao watateuliwa na kompyuta kupitia mfumo wa pata potea.
Alisema serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba nafuu katika mitaa ya Shauri Moyo, Starehe na Kibera B jijini Nairobi.
“Katika mtaa wa Shauri Moyo serikali inajenga nyumba 8,500 na inanuia kujenga nyumba 4,400 mtaani Kibera. Tumeanza harakati za kusaka ardhi ya kujenga nyumba katika Kaunti 25 ambazo zimetia saini mkataba wa kutakakujumuishwa katika mradi wa kitaifa wa utoaji wa nyumba nafuu,” akasema Bw Oguna.