Habari Mseto

Mbadi, Duale wakutana na balozi Kyle McCarter

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi amewataka wabunge kupitisha haraka mswada wa kufanikisha mageuzi katika mfumo wa uchaguzi nchini.

Akiongea na wanahabari Alhamisi baada ya kukutana na balozi wa Amerika nchini Kyle McCarter, Bw Mbadi amesema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa kufanyiwa mageuzi wakati huu ambapo kuna utulivu wa kisiasa nchini ili kuzuia mivutano kama iliyoshuhudiwa mwaka 2017.

“Wakati ambapo kuna utulivu katika mandhari ya siasa ndipo mageuzi mwafaka yanapaswa kufanywa kwa IEBC ili iweze kusimamia uchaguzi mkuu ujao kwa njia huru na yenye uwazi. Haya ndiyo baadhi ya masuala ambayo nimejadili na balozi wa Amerika,” akasema afisini mwake katika majengo ya bunge, Nairobi.

Kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa, John Mbadi. Picha/ Hisani

Tayari Kamati ya Bunge kuhusu Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC) inashughulikia mswada wa marekebisho ya sheria ya IEBC.

Mswada huo, miongoni mwa mambo mengine, unalenga kutenganisha kabisa majukumu ya makamishna na sekritarieti ili kuondoa mgongano ulioshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Kupunguza idadi ya makamishna

Aidha, mswada huo unalenga kupunguza idadi ya makamishna kutoka saba hadi watano huku idadi ya chini ya makamishna wanaohitajika kupitisha maamuzi makuu ikipunguzwa kutoka watano hadi watatu.

Baadaye balozi McCarter alifululiza hadi afisini mwa kiongozi wa wengi Aden Duale kwa mashauriano ya faragha.

Baada ya mkutano huo, Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini, amewaambia wanahabari kwamba walijadili namna mabunge ya Kenya na Amerika yanaweza kushirikiana katika masuala ya utungaji sheria.

“Tumejadiliana na balozi Kyle kuhusu jinsi bunge letu linaweza kushirikiana na lile la Uingereza kama njia ya kuendeleza ushirikiana kati ya mataifa hayo mawili,” akasema.

Bw Duale ametumia fursa hiyo kutangaza kuwa Julai 2019 yeye na Bw Mbadi watazuru Bunge la Congress nchini Amerika ili “kujifahamisha na mitindo na kanuni za bunge hilo.”