MakalaSiasa

MOSES KURIA: Hachoki kujikwaa ulimi kila mara akitafuta lango la Ikulu

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria akiwakilisha kijiji ambacho kina boma la Rais Uhuru Kenyatta cha Ichaweri sio mgeni kwa wengi hapa nchini.

Sasa anasema kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 na ambapo anakiri kuwa “hata nikianguka kura hiyo sitaanguka kwa kitanda cha mtu eti nitamzuia kufurahia usingizi wake.”

Hivi majuzi akiwa mfuasi sugu wa uwaniaji wa urais wa Naibu wa Rais, William Ruto, siku hizi amemgeuka na amemuonya kimamlaka kuwa “kiburi chako kitakunyima urais.”

Ni wazi kuwa serikali ya rais Kenyatta ilipopata fursa ya kupendekeza ni nani atwae ubunge wa Gatundu Kusini katika Uchaguzi mdogo wa Agosti 7, 2014, ilimpendekeza Kuria ikiwa na matumaini kuwa yeye ndiye alikuwa mradi mwafaka wa kuwa na Raila Odinga wao.

Katika mtazamo huo, serikali haikujaribu kuficha nia yake kuwa ilikuwa ikimtegemea Kuria kuwa mjeledi wa kuadhibu na kunyamazisha Odinga ambaye kila mara alikuwa amejipa umaarufu wa mazoea ya kuzua tumbo joto ya kisiasa kufuatia weledi wake wa kucheza siasa.

DP Ruto alikuwa muwazi kabisa kuhusu nia ya serikali kumpata B Kuria kama mbunge aliposema katika kampeni Mjini Gatundu kuwa “tunamtaka mbunge mpya wa eneo hili awe ni mtu ambaye anajua kujibizana na upinzani.”

Ni katika hali hiyo ambapo Kuria alionyeshwa uungwaji mkono kwa kiwango kikuu na mrengo wa Jubilee ambapo hata ingawa alishindwa katika mchujo na Bi Joyce Wanjiku ambaye ni mjane wa aliyekuwa mbunge wa eneo hilo kabla ya kuaga dunia, Bw Joseph Ngugi, Kuria alipewa cheti cha uwaniaji.

Juhudi za kuwasilisha malamishi yake kwa jopo la kutatua mizozo ya kindani ya TNA ziligonga mwamba na Bw Kuria akasisitizwa kuwa ndiye mpeperushaji wa bendera ya serikali katika eneo hilo.

Lakini swali ambalo wachanganuzi wa kisiasa wanawaza juu yake ni ikiwa Kuria ameweza kutimiza wajibu huo katika kipindi chake cha miaka mitano ambayo amekuwa mbunge wa Gatundu Kusini.

Ndani kila mara

Katika kutekeleza wajibu huo wa kumdhibiti Odinga, kile Kuria amezoa katika makabiliano hayo ni kutupwa kwa seli mara kadhaa kwa madai ya uchochezi na kufikia sasa anaandamwa na kesi tatu mahakamani za uchochezi.

Kuria alijiunga na siasa mwaka wa 2007 na ni mhimili wa Shahada ya uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi alichopata mwaka wa 1993.

Bw Kuria aliajiriwa mara yake ya kwanza mwaka wa 1994 katika kampuni ya Mafuta ya Total na kisha akahamia hadi Benki ya Standard Chartered kama mpanga ratiba wa sera za uwekezaji.

Aidha, alihamia benki ya Al Rajhi Nchini Saudi Arabia kama mkurugenzi wa mawasiliano ya kiteknolojia lakini hatimaye akazindua kampuni yake ya uhusiano mwema na masuala ya utangazaji mwaka wa 2003.

Alijiunga na siasa mwaka wa 2007 alipochukua wadhifa wa Mkurugenzi wa ratiba za kampeni za Rais mstaafu Mwai Kibaki na baada ya ushindi, akachaguliwa kama msemaji wa chama cha PNU chake mzee Kibaki.

Mkurugenzi wa masuala ya kidijitali katika Ikulu Bw Dennis Itumbi anamtambua Bw Kuria “kama kiungo muhimu katika mapambano ya kisiasa na aliye na uwezo wa kuleta mtazamo mpya katika kila changamoto.”

Aidha, anamlimbikizia Kuria sifa kama mzoeefu wa umakinifu katika kutoa tathmin kuhusu siasa za malumbano.

Umuhimu wake

Bw Gasper Odhiambo ambaye ni mdadisi wa kisiasa anasema kuwa umuhimu wa Kuria katika siasa za Jubilee umejiangazia katika hali kadhaa.

“Nia kuu ya mrengo wa Jubilee kumuunga mkono Kuria imefanikiwa pakubwa kwa kuwa ilikuwa ni kupata mtu anayejulikana kutokuwa na uoga wa kuongea hadharani, aliye na ari ya ubishi na ambaye hatimaye angetumika kuongoza mapambano dhidi ya upinzani,” asema.

Anasema kuwa mrengo wa serikali ulimwafikia Bw Kuria kupitia juhudi zake za kupambana na wimbi kali lililozushwa na Odinga alipoamua kuandaa mkutano wa Sabasaba Jijini Nairobi akitaka serikali iandae mdahalo wa kitaifa wa kutafuta jibu kwa changamoto chungu nzima za utawala zinazomtatiza Mkenya wa Kawaida.

“Kuria kwa haraka alitangaza kuwa mdahalo huo ungeandaliwa lakini ni lazima wafuasi wa Jubilee wangemtembelea Odinga kwake nyumbani ili awafafanulie zaidi kuhusu masuala aliyotaka yatafutiwe suluhu. Kuria alitangaza kuwa tayari alikuwa ameandaa wafuasi milioni moja wa kumtembelea Odinga katika mtaa wa Karen, Kaunti ya Nairobi siku ya mkutano wa Saba Saba ya 2017,” asema.

Odhiambo anasema kuwa tukio hilo lilifanya idara za usalama kuzima mikutano hiyo na pia serikali ikapata afueni kubwa ya siasa kuchafuka.

Utata huo wa Bw Kuria alizua taharuki katika mrengo wa upinzani kiasi kwamba Odinga mwenyewe aliomba maafisa wa usalama walinde mkutano wake usisambaratishwe na Jubilee.

Kafara

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa siasa Festus Wangwe, Kuria “ni kibarakala au kifaa tu cha serikali ambacho hupendwa kwa kuwa na moyo wa kujitoa kafara kwa imani yake ya kisiasa na ambapo katika siku za hivi majuzi, kimekosa kazi kufuatia salamu za maridhiano kati ya Rais na Odinga.”

Anasema kuwa Bw Kuria hawezi kungoja apate mtazamo mwafaka kuhusu suala lolote la kisiasa na ataruka kutoa vipande vya ubishi bora tu anatetea alio na imani nao kisiasa.

Hata hivyo, Wangwe anasema kuwa malipo kwa serikali ya Rais Kenyatta ni kuwa, Kuria ameishia kuisababishia kila aina ya changamoto kwa kuwa “amekuwa na mtindo wa kujikwaa ulimi anapotoa matamshi yake ya kisiasa.”

Na sasa, ndiye huyo anasaka kuwa Rais wa tano wa Kenya, na apate asipate, atakumbukwa kama mwanasiasa wa kipekee ambaye hata hukiri hadharani kuwa “napenda pombe kama maziwa.”