• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kalonzo hafai urais 2022, Musila ashikilia

Kalonzo hafai urais 2022, Musila ashikilia

Na PIUS MAUNDU

ALIYEKUWA Seneta wa Kitui David Musila ameirai jamii ya Akamba kutomuunga mkono kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, akisema kuwa hatafaulu kwenye nia yake ya kuwania urais mnamo 2022.

Bw Musila alisema kuwa Bw Musyoka hajafaulu kwenye azma yake ya kuwania kwa mara kadhaa sasa, hivyo jamii hiyo haitafaidika kwa vyovyote vile ikiwa itaendelea kumuunga mkono.

“Tumejaribu kuwania urais mara tatu kwa kumuunga mkono mmoja wetu na hatujafaulu. Imefikia wakati tubadili mbinu.

“Uamuzi pekee tulio nao kama jamii ni kukubali kumuunga mkono aliye na uwezekano mkubwa kushinda. Hilo ndilo litatuwezesha kupata nyadhifa kuu serikalini. Hivyo ndivyo tungefanya katika uchaguzi uliopita lakini tulipotoshwa,” akasema, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Alhamisi.

Hata hivyo, hakufafanua kuhusu “kiongozi aliye na uwezekano mkubwa” kushinda.

Bw Musila, hata hivyo, alieleza kuwa Bw Musyoka hapaswi kuongoza chama kitakachoibuka mshindi kwani hana idadi ya kutosha ya wapiga kura wanaoweza kumwezesha kutwaa urais. Mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa miongoni mwa waandani wakuu wa Bw Musyoka kabla ya tofauti kali kuibuka baina yao.

Alimlaumu Bw Musyoka kwa kuwazuia wanasiasa wanaochipukia kueneza mabawa yao ya kisiasa, lengo lake kuu likiwa kuendelea kuidhibiti jamii ya Akamba kisiasa.

Alisema kuwa huenda hilo likaizuia jamii hiyo kujiunga na muungano wa kisiasa utakaoibuka mshindi.

Bw Musila alikihama chama cha Wiper mnamo 2017 baada ya kushindwa kwenye uteuzi na Dkt Julius Malombe ambaye alikuwa gavana wa kaunti hiyo. Aligombea ugavana lakini akashindwa na Bi Chariry Ngilu, aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Narc.

Bw Musila alimlaumu Bw Musyoka kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi, hali iliyomfanya kushindwa.

Bw Musila hata hivyo aliunga mkono nia za urais za magavana Kivutha Kibwana wa Makueni na mwenzake wa Machakos, Alfred Mutua.

Wiki tatu zilizopita, Prof Kibwana alimwambia Bw Musyoka kufutilia mbali nia yake ya kuwania urais mnamo 2022.

“Tumemuunga mkono Kalonzo tangu 1993. Kila wakati anapogombea ama kuunga mkono muungano wa kisiasa huwa hafaulu. Tutautuma ujumbe wa wazee, wanawake na vijana kumwambia kwamba wakati wetu wa kuwania umefika. Anapaswa kutuunga mkono,” akasema Prof Kibwana. Tangazo lake lilipokelewa kwa hisia tofauti.

Licha ya hayo, Bw Musyoka amekuwa akipuuzilia mbali kwamba amepoteza urais mara nyingi. Amesisitiza kwamba atawania urais tena mnamo 2022, ambapo mara hii hatamuunga mkono mgombea yeyote.

Akiwahutubia wafuasi wake katika eneo la Ikonyo, Makueni, Bw Musyoka alisema kuwa haitakuwa bora kwake kumuunga mkono mgombea yeyote.

Alisifia uhusiano wake mzuri na Rais Uhuru Kenyatta, akisisitiza kuwa ndiye anayefaa zaidi kuwa rais wa tano wa Kenya.

You can share this post!

Walimu walia kulemewa na mtaala mpya wa mafunzo

Upinzani Sudan wakataa mazungumzo na wanajeshi

adminleo