• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Mamapima awatuza walevi sugu unga na mafuta

Mamapima awatuza walevi sugu unga na mafuta

Na MWANDISHI WETU 

KITHUNGUINI, MACHAKOS

Mamapima mmoja maarufu sokoni hapa, alionyesha ukarimu usiomithilika alipoamua kuwanunulia wateja wake wa kila siku paketi mbili za unga na mafuta ya kupikia kama shukrani kwa kulewa kila siku.

Kulingana na mdokezi, mamapima huyo alifungua biashara hiyo miaka miwili iliyopita na ikavuma faida mno.

Makastoma wa karibu na mbali walikuwa wakifurika katika maskani yake kubugia mvinyo mpaka chee.

“Baa hiyo iliangamiza nyingine sokoni hapa. Hii ilichangiwa na huduma mufti za mama huyo na wafanyakazi wake pamoja na mapokezi muruwa,’’ alisema mpambe wetu.

Inasemekana kwamba, wakulima wa kahawa wakilipwa bonasi yao, wale wa mboga na matunda wakiuza mazao yao na vibarua wakipokea ujira wao, walikuwa wakifululiza moja kwa moja hadi kwa mama pima huyo kujipanguza jasho kwa kubugia mvinyo.

Hii ilimfanya awe mkwasi kwa kutia kibindoni donge nono kila siku. Twaarifiwa kwamba, mamapima huyo alikata kauli ‘kurudisha mkono’ kwa walevi hao wa dhati na akawanunulia kila mmoja paketi mbili za unga wa ngano na mafuta ya kupikia ili wapelekee familia zao.

“Mmenipiga jeki na kunisapoti tangu nilipofungua baa hii. Mmekuwa mkilewa kila siku na kunipatia faida nono. Kwa hivyo, nimeamua kuwanunulia unga na mafuta kama shukrani zangu kwenu,’’ alisema mama pima huku akishangiliwa kwa nderemo na vifijo na walevi hao.

Hata hivyo, licha ya walevi hao kununuliwa bidhaa hizo, baadhi yao hawakuzifikisha nyumbani, bali waliziuza kwa bei duni mitaani ili wapate hela za kugharamia dozi yao walivyozoea.

Duru zaarifu kuwa, ukarimu huo ulimjenga mno mama huyo kibiashara kwani baada ya siku hii waliendelea kubugia dozi kwake kwa wingi huku wakati mwingine wakikesha humo.

You can share this post!

Upinzani Sudan wakataa mazungumzo na wanajeshi

TAHARIRI: Sheria kali kuhusu noti mpya zikazwe

adminleo