AFYA NA USAFI: Faida za kuoga kwa maji baridi
Na MARGARET MAINA na MASHIRIKA
WATU wengi hupenda kuogea maji moto, hii ni kutokana na kuogopa ya baridi au sababu za kimazoea tu.
Hata hivyo, maji baridi yana manufaa mengi zaidi.
Hufanya mtu achangamke
Mara nyingi mtu anapooga akitumia maji ya baridi hasa baada ya kuamka, humfanya awe katika hali nzuri ya kuwa tayari kuendelea na majukumu yake.
Hulainisha ngozi na nywele
Maji moto huchibua ngozi na nywele hasa kwa kuondoa mafuta laini yanayolinda ngozi na nywele na kuvifanya viwe vikavu.
Kwa kuogea maji ya baridi, ngozi na nywele zako zitaachwa katika hali nzuri ya kupendeza.
Huchangia katika afya ya misuli
Wanamichezo wanafahamu kuwa kuogea maji baridi baada ya michezo au mazoezi huwafanya wajisikie vizuri. Hili ni kutokana na maji baridi kuhamasisha mzunguko wa damu ambao huiwezesha misuli kujijenga tena upya vyema.
Hukusaidia kulala vyema
Je, umeshawahi kuogea maji baridi ukiwa umechoka sana au umefanya kazi ngumu? Kama umeshawahi kuogea maji baridi baada ya kujipata katika hali hizo ni wazi kuwa ulijisikia vizuri na ukalala vizuri pia.
Huboresha mzunguko wa damu
Mtu anapooga kwa maji baridi, mapigo ya moyo huenda kasi na kusababisha damu kuzunguka vyema kwenye maeneo mbalimbali ya mwili. Mzunguko mzuri wa damu utaondoa vile visivyotakiwa na kuleta vile vinavyotakiwa kwenye viungo na sehemu mbalimbali za mwili wako.
Hurudisha nguvu za mwili
Mara nyingi mtu anapokuwa amechoka, kwanza huhitaji kuoga ili ajisikie vizuri. Ni wazi kuwa mtu anapooga hasa kwa maji baridi hujisikia kurudiwa na nguvu au hali nzuri kuliko ile aliyokuwa nayo kabla ya kuoga.