AFYA: Manufaa ya kula embe
Na MARGARET MAINA
EMBE ni tunda linalofahamika na kupendwa na watu wengi.
Watu hula tunda hili moja kwa moja au kulitumia kutengeneza juisi.
Huboresha metaboli
Embe ni tunda lenye nyuzinyuzi kwa kiasi kikubwa.
Nyuzinyuzi zinahitajika sana katika kufanya mchakato wa metaboli kwenda vizuri.
Huboresha afya ya macho
Kula embe kutakunufaisha kwa kulinda macho yako dhidi ya kudhoofu kwa misuli ya macho.
Embe ni chanzo kizuri cha Vitamini A ambayo ni muhimu kwa ajili ya macho.
Hukabili shinikizo la damu mwilini
Madini ya potassium yanayopatikana kwenye embe huasidia dosari zinazosababishwa na madini ya sodiamu katika damu.
Potassium hurekebisha nguvu ya msukumo wa damu (blood pressure) na kuufanya uwe wa kawaida.
Hutumika kama kipodozi cha nywele
Kwa kuchanganya ujiuji wa embe, yai pamoja na kijiko kimoja cha asali, na yoghurt; unaweza kupata kipodozi kizuri kwa ajili ya nywele zako.
Paka mchanganyiko huu na subiri kwa muda wa dakika thelathini kabla ya kuosha nywele zako.
Hupunguza lehemu (cholesterol) mwilini
Kiwango cha mafuta ya lehemu kikizidi ni hatari kwa ajili ya afya ya moyo.
Vitamini C pamoja na pectin inayopatikana kwenye embe huuwezesha mwili kujikinga na athari za lehemu.
Ni chanzo kizuri cha madini ya chuma
Embe ni chanzo kizuri cha madini ya chuma ambayo ni muhimu kwako ili kujikinga na maradhi kama vile anemia.
Huboresha kinga ya mwili
Kinga mwili inahitaji vitamini A na C ili kujijenga na kujiimarisha. Hivyo ulaji wa maembe utakupatia vitamini hizi zinazopatikana kwenye matunda haya kwa wingi.
Ni chanzo cha asidi ya folic
Asidi ya folic inayopatikana kwenye embe katika mfumo wa vitamini B ni muhimu sana kwa afya ya mama mjamzito na mtoto. Inashauriwa na wataalamu wa afya kula tunda la embe hasa kwa wajawazito.
Huboresha mmeng’enyo wa chakula
Embe lina enzyme ambazo husaidia katika uvunjwaji na uchakatwaji wa protini mwilini. Pia embe lina nyuzinyuzi ambazo ni muhimu katika kumeng’enya chakula.
Husaidia katika afya ya ngozi
Embe ni muhimu kwa ajli ya afya ya ngozi kwani lina beta-carotene ambayo mwili huibadili kuwa vitamini A na lina vitamini C kwa wingi ambazo zote kwa pamoja ni muhimu kwa ajili ya afya ya ngozi.