• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Washukiwa wawili wa uwindaji haramu wanaswa Nakuru

Washukiwa wawili wa uwindaji haramu wanaswa Nakuru

Na PHYLIS MUSASIA

POLISI wa Nakuru pamoja na maafisa wa KWS Alhamisi jioni walinasa pembe 16 za ndovu katika mtaa wa Pipeline.

Kulingana na kamanda wa polisi kwenye kaunti hiyo Bw Stephene Matu, washukiwa wawili ambao ni baba na mwanawe walitiwa mbaroni baada ya polisi kufahamishwa na wakazi wa Pipeline habari za kutatanisha kuhusu mienendo za wawili hao kwenye mtaa huo.

Polisi na maafisa was KWS wakionyesha vipande 16 vya pembe za ndovu mtaani Pipeline, Nakuru. Picha/ Phylis Musasia

Bw Matu alisema washukiwa walionekana wakizurura bila ya kuwa na mwelekeo thabiti kwenye mtaa huo huku wakitumia gari aina ya Toyota Fielder lenye nambari za usajili KCG 552N.

“Wakazi wa eneo hili walipowaona washukiwa wakiendesha gari lao na kupita kila njia huku wakionyesha tabia za kutokuaminika, walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Pakawa.” amesema Bw Matu.

Baadaye, Bw Matu amesema, wawili hao walikamatwa na polisi wakiwa katika nyumba moja ya kukodisha ambapo walipatikana wakiwa na pembe hizo pamoja na magunia mawili ya makaa.

“Tulipowauliza maswali, ilitambulika kuwa washukiwa hao walikuwa wamesafiri kutoka mjini Eldoret na hadi hapa Nakuru ambapo walitarajia kupatana na mnunuzi ambaye alikuwepo njiani kutoka jijini Nairobi,” akaongeza Bw Matu.

Afisa mmoja wa KWS Bi Catherine Wambani amesema ni jambo la kushangaza kuona jinsi wanyama wa porini ambao wananufaisha nchi kwa kiwango kikubwa kiutalii, wanavyouawa kioholela ili kunufaisha mahitaji ya watu binafsi,” akasema Bi Wambani.

Aliongeza: “Hii ina maana kuwa takribani ndovu wanane waliuawa ili wawindaji haramu kupata pembe hizi 16. Wananchi wasipokuwa waangalifu, miaka ijayo tutawakosa hawa wanyama ambao wangesaidia vizazi vijavyo.”

Wawili hao wanaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Pakawa huku uchunguzi wa kina ukiendelea.

You can share this post!

Mwanamume aliyepatikana na hatia ya kunajisi wasichana...

SOKA MASHINANI: Klabu ya Thika Sporting FC

adminleo