Joho, Matiang'i tiketi tosha?
Na CHARLES LWANGA
BAADHI ya wabunge wa kutoka Kaunti za Pwani wamejitenga na wito wa kumuidhinisha Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho kuwa msemaji wa eneo la Pwani na pendekezo la kumteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuwa mgombea-mwenza.
Mzozo umezuka huku baadhi ya wabunge wakitaka Gavana wa Kilifi Amason Kingi kuwa mgombeaJI WA urais wa eneo la pwani.
Wabunge waliohudhuria sherehe za Eid al-Fitr mnamo Jumatano mjini Mombasa, walimuidhinisha Bw Joho kuwa mgombea urais wa eneo la Pwani na kupendekeza amteue Dkt Matiang’i ambaye alikuwepo katika hafla hiyo, kuwa mgombea mwenza.
Wanaomuunga Gavana wa Kilifi Amason Kingi walikashifu wenzao wa Bw Joho wakisema walisaliti wakazi wa Kaunti ya Kilifi.
Kulingana na Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya wabunge wa Kilifi wanapaswa kuongea kwa sauti moja nyuma ya Bw Kingi.
Wakati wa hafla ya Eid, Mbunge wa Kilifi Kusini, Bw Ken Chonga alimpigia debe Bw Joho akisema ndiye anayefaa kuwa mgombeaji urais wa eneo la Pwani na kumtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuwa naibu wake.
Akizungumza eneo la Gede katika mkutano wa hadhara wa kuandaa bajeti ya Kaunti uliofanyika mnamo Alhamisi, Bw Baya alisema kuwa Kaunti ya Kilifi itajiamulia yenyewe mgombeaji wa urais katika uchaguzi wa 2022.
Bw Baya alishangaa ni kwa nini wabunge wengine hawawezi kuunga viongozi wa kaunti yao badala ya kwenda Mombasa kuhudhuria sherehe za Eid kumpigia Bw Joho debe kama mgombezi wa urais kwenye uchaguzi wa 2022.
Wakati wa sherehe za Eid al-Fitr, Bw Chonga alisema kuwa Bw Joho atakuwa mgombeaji urais wa eneo la Pwani kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo akiwemo Waziri wa Utalii Najib Balala pia walimuunga Bw Joho na kumtaka aunganishe magavana wa Pwani kuelekea 2022.
“Uamuzi wa kila Mpwani unajulikana, mwaka wa 2022 hatutapigia debe mgombeaji wa urais kutoka maeneo mengine. Wacha wanaozungumza maneno yasiyofaa waseme lakini sisi tuna rais wetu hapa,” alisema.
Imani
Bw Chonga alisema kuwa Rais Uhuru Kenyatta tayari ameonyesha imani na Bw Matiangi’ kwa kumpa majukumu muhimu kama kusimamia wizara zote serikalini.
“Nakwambia ndugu yangu Sultani, tunapokupa jukumu la kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya, hakikisha naibu wako atakuwa Bw Matiangi’ kwa sababu ana uwezo. Tumemjaribu na tunaona ana uwezo,” alisema.
Lakini Bw Baya alimkashifu Bw Chonga kwa kupigia debe viongozi wengine badala ya kutumia wakati wake na Bw Matiangi’ kutafuta suluhisho la dhuluma za mashamba eneo la Kilifi.
“Badala ya kumweleza kufurushwa kwa wakazi eneo la Kilifi Kusini kutoka mashamba yao, unamwambia jinsi anavyofaa kuwa Naibu Rais. Pia mimi nilikuwa nimeitwa kuhudhuria hafla hiyo lakini sikuenda,” alisema na kuuliza, “Kwa nini kiongozi aende kuitikia mwaliko wa Bw Joho badala ya kuwa mwaminifu kwa kiongozi wake wa Kilifi.”
Baadhi ya wabunge ambao wangali waaminifu kwa Gavana Kingi ni Bw Baya, Mbunge wa Magarini Michael Kingi, Bi Aisha Jumwa (Malindi), Bw Paul Katana (Kaloleni), Seneta Stewart Madzayo na mwakilishi mwanamke Gertrude Mbeyu. Wabunge wa Kilifi ambao wamekuwa wakimpigia debe Bw Joho ni Bw Chonga, mbunge wa Ganze Teddy Mwambire na mwenzake wa Rabai William Kamoti.