• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 9:55 AM
Kenya yailemea Madagascar 1-0 katika mechi ya kirafiki jijini Paris

Kenya yailemea Madagascar 1-0 katika mechi ya kirafiki jijini Paris

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilianza mechi zake za kirafiki za kujiandaa kwa Kombe la Afrika (AFCON) kwa ushindi baada ya kuchabanga Madagascar 1-0 Ijumaa usiku uwanjani Robert-Bibin jijini Paris nchini Ufaransa.

Hata hivyo, Harambee Stars, ambayo inashikilia nafasi moja nyuma ya wanavisiwa hao kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) katika nafasi ya 108, haikupata ufanisi huu kwa urahisi.

Iliponea tundu la sindano kujipata bao moja nyuma pale Madagascar ilipata penalti katika kipindi cha kwanza, lakini kipa Patrick Matasi alikuwa macho kudaka penalti hiyo. Faneva Ima Andriatsima alifanyiwa madhambi na Matasi ndani ya kisanduku dakika ya 43.

Hata hivyo, kipa bora wa Kenya mwaka 2016 na 2017 Matasi alirekebisha kosa lake kwa kunyaka penalti kutoka kwa mshambuliaji Charles Carolus Andriamahitsinoro.

Beki wa kupanda na kushuka wa Madagascar Romain Metanire alikuwa mwiba kwa Stars pembeni kulia.

Alisaidia vijana wa kocha Nicolas Dupuis kupata nafasi kadha nzuri, lakini walinzi wa Kenya walikuwa imara kuwazima.

Kikosi cha Madagascar. Picha/ Hisani

Kenya iliona lango dakika ya 52 kupitia kiungo wa Tottenham Hotspur, Victor Wanyama, ambaye alifuma penalti kwa ustadi mkubwa.

Beki wa Madagascar Jeremy Michel Morel alinawa mpira ndani ya kisanduku chao na kumpa nahodha huyo wa Stars fursa muhimu ya kuleta utofauti katika mechi hiyo ya kwanza ya Kenya ya kirafiki.

Victor Wanyama (kulia) baada ya kufunga penalti. Picha/ Hisani

Barea, jinsi timu ya taifa ya Madagascar inafahamika kwa jina la utani, iliingia mechi ya Kenya ikiwa tayari imeshasakata mechi moja ya kirafiki. Ilitoka 3-3 dhidi ya wenyeji wake Luxembourg mnamo Juni 2.

Baada ya kukamilisha mechi zake za kirafiki, Madagascar itarejea nchini mwao Juni 9 kwa mapumziko mafupi na kisha kukutana na raia wa nchi hiyo uwanjani Mahamasina hapo Juni 10.

Kenya kwa upande wake imekita kambi ya mazoezi jijini Paris; kambi ya siku 19.

Baada ya kupimana nguvu dhidi ya Madagascar, Stars inatarajiwa kuvuka mpaka na kuingia jijini Madrid nchini Uhispania kwa mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itakayosakatwa Juni 15.

DR Congo inatarajiwa kutoa ushindani mkali zaidi kwa Stars, hasa kutokana na uzoefu wa wachezaji wake katika AFCON na mashindano mengine ya Bara Afrika yakiwemo yale ya Klabu Bingwa na Kombe la Mashirikisho.

‘The Leopards’ ya Congo pia inajivunia kuwa nafasi 62 mbele ya Kenya katika nafasi ya 48 duniani.

Baada ya kulimana na DR Congo, Kenya itaelekea nchini Misri kwa kindumbwendumwe cha AFCON hapo Juni 19. Vijana wa Migne, ambao wanarejea katika AFCON tangu mwaka 2004, wametiwa katika Kundi C ambalo linajumuisha Senegal, Algeria na Tanzania.

Dimba la AFCON limeratibiwa kuanza Juni 21 na kumalizika Julai 19.

Mechi za Kundi C zitachezewa jijini Cairo. Jumla ya mataifa 24 yatashiriki makala ya mwaka 2019. DR Congo na Madagascar pia ziko katika AFCON.

Madagascar iko katika Kundi B ambalo linawakutanisha dhidi ya Nigeria, Guinea na Burundi. Madagascar na Burundi zinashiriki AFCON kwa mara yao ya kwanza katika historia ya mashindano haya.

DR Congo itapepetana na Misri, Uganda na Zimbabwe katika Kundi A. Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini na Namibia zinaunda Kundi D nazo Tunisia, Mali, washiriki wapya kabisa Mauritania, na Angola wako Kundi E.

Mabingwa watetezi Cameroon pamoja na Ghana, Benin na Guinea-Bissau wanakamilisha orodha ya washiriki baada ya kukutanishwa katika Kundi F.

You can share this post!

SOKOMOKO: Tenda wema

Mhubiri aliyeshtakiwa kwa wizi wa hundi ageuza mahakama...

adminleo