DAU LA MAISHA: 'Heri ya kijungujiko kuliko 'ombaomba'…'
Na PAULINE ONGAJI
UNAPOTAZAMA ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Facebook, ni rahisi kudhani ni msichana wa kawaida mwenye umri wa miaka 21.
Hii ni kutokana na picha zake alizochapisha, zinazomuonyesha akiwa anapendeza kwa mavazi ya mtindo wa kisasa na vipodozi vya kuvutia.
Lakini usipumbazwe na muonekano huo kwani huku baadhi ya wasichana wa umri wake wakitumia picha za aina hii kama chambo cha kuwanasa masponsa kufadhili maisha yao ghali, Anitah Mbugua anatia bidii katika sekta ambayo kwa wengi haiwafai vijanajike wa leo.
Msichana huyu amekiuka dhana za kiumri na kijinsia kujitafutia riziki katika taaluma ambayo wengi wanaichukulia kuwa ya kiume.
Bi Mbugua ambaye pia ni mwanafunzi wa uhasibu katika Chuo Kikuu cha Kenya Polytechnic jijini Nairobi, anafanya kazi ya kusambaza keki katika maduka mbalimbali kwa kutumia pikipiki; boda boda au ‘nduthi’ kama inavyofahamika kwa lugha ya mtaani.
Ni kazi ambayo imemfanya kupewa jina ‘nduthi girl’, msichana anayeendesha pikipiki.
Kila alfajiri, Bi Mbugua hurauka tayari kuanza kibarua chake kinachompeleka katika maduka mbalimbali katika mitaa ya Dagoretti, Kirigu na Karen, jijini Nairobi.
“Siku yangu huanza saa kumi na moja alfajiri na jukumu langu huwa kusambaza bidhaa hizi katika maduka kadha hadi saa nane alasiri kisha naelekea chuoni,”anaeleza.
Kuna siku ambazo yeye hufanya kazi hii kwa kutumia pikipiki huku zingine akitumia gari.
Japo amewahi kukumbana na kejeli kutokana na ajira hii, ni kazi ambayo anasema anaipenda sana na imemsaidia kuchangia mahitaji ya kifedha ya familia yake. “Sikuacha kejeli zinifishe moyo kwani kila nilipokuwa nikirejea nyumbani nilikumbuka kwamba nafanya kazi kujiendeleza kimaisha na kukamilisha masomo yangu,” aeleza.
Ni kazi alijifunza akiwa katika darasa la nane huku mamake ambaye pia zamani alikuwa akiendesha pikipiki, akiwa kigezo chake kikuu.
“Kujifunza huku kuliniwezesha kumsaidia mamangu wakati wa mapumziko na likizo,” anaeleza.
Ari yake pia ilichochewa na haja ya kutaka kujitafutia kipato na hivyo kujitegemea.
“Tangu utotoni nilikuwa na msukumo wa kujitafutia pesa badala ya kumtegemea mtu mwingine kukidhi mahitaji yangu, hasa baada ya kuona bidii ya mamangu,” anaeleza.
Lakini usidhani mambo yamekuwa shwari hasa baada ya kupuuza bezo na kejeli alizokumbana nazo. Anasema asingalikuwa na nidhamu, ukakamavu na bidii, asingaliweza kusawazisha kazi hii na masomo.
“Kazi hii inahitaji muda na nguvu nyingi kumaanisha kwamba wakati mwingine unafika shuleni ukiwa umechoka. Lakini nidhamu, vilevile kujituma ndivyo vimekuwa siri kuhakikisha kwamba namaliza kazi yangu kwa wakati ufaao, na hata kupata muda wa kwenda darasani,” anaeleza.
Ukakamavu wake umemfanya kuwa penzi kwa wateja wengi anaowahudumia.
“Lakini pia ari yangu inatokana na heshima kuu ninayopokea kutoka kwa wateja wengi wanaofurahishwa na kazi na ujasiri wangu,” anasema.
Bidii yake aidha imemzolea heshima sio haba hasa miongoni mwa wanafunzi wenzake.
Mawaidha yake kwa wasichana na wanawake kwa jumla ni kutochagua kazi kwa msingi wa kijinsia.
“Kazi ni kazi mradi mwisho wa siku unapata riziki yako halali. Afadhali ufanye kazi inayokuhakikishia kipato kutokana na jasho lako badala ya kutegemea mifuko ya watu ambapo mara nyingi utajipata pabaya,” anashauri.