FUNGUKA: 'Usinifuatefuate ikiwa unanuka shombo'
Na PAULINE ONGAJI
KWA wanawake wengi, kuambatana na vigezo wanavyoweka kabla ya kumchagua mchumba au mume, usafi huwa si miongoni mwa mambo makuu wanayoangalia.
Hii ni tofauti sana na Jane, 37.
Usafi wa mwili tena wa kupindukia ndo kigezo chake kikuu anachoangalia kabla ya kuamua kwamba kaka anatosha kumchumbia.
Jane, anamiliki baa katika mojawapo ya mitaa ya kifahari.
Japo hana kisomo cha hali ya juu, pamoja na nduguze, walibahatika kwani wanatoka katika familia yenye utajiri mkubwa, na baba yao alipofariki miaka kumi iliyopita, aliwaachia mihela ya kutosha.
Kwa hivyo, mbali na kurithi jumba kubwa katika mojawapo ya mitaa ya kifahari, pia alipata baa hiyo ambayo amekuwa akiiendesha kwa miaka saba sasa.
Kutokana na hili, Jane hana tatizo la kifedha kwani anapokea mapato mazuri kutoka kwa biashara hiyo, vilevile hana majukumu mengi ya kifedha.
Mbali na hayo mambo ya kawaida, Jane anapenda usafi sana kiasi kwamba yeye hubadilisha mtindo wa nywele kila wiki.
Usafi huu ameueneza pia katika masuala ya mahaba ambapo vigezo vyake vimekuwa vikiwaacha wengi vinywa wazi.
“Lazima kidume awe safi kupindukia tokea utosini hadi miguuni.
Lazima aoge angaa mara tatu kwa siku na asugue meno kila baada ya kula chochote. Hii inamaanisha kwamba, ikiwa anataka kuwa mpenzi wangu, basi lazima ajiandae kutembea na mswaki na dawa ya meno mkobani.
Lazima kila wakati viatu vyake ving’ae, kumaanisha kwamba ikiwa hawezi kumudu gharama ya kupata huduma za kupigiwa viatu rangi mjini, basi atembee na brashi na rangi ya viatu.
Pia, lazima kucha zake ziwe shwari kila mara. Sipendi kuona kaka mwenye kucha chafu na ndefu kiholela.
Kimavazi, lazima usafi huu pia udumishwe. Kwa mfano, lazima ubadilishe soksi kila siku. Boksa lazima ibadilishwe mara mbili kwa siku. Isitoshe, kila baada ya miezi mitatu lazima utupe hizo boksa mzee na ununue mpya.
Shati pia utabadilisha mara mbili kwa siku kwani mimi hukerwa sana kila ninapokumbana na dume lenye shati lililojichora majasho kwapani.
Katika masuala ya nywele, lazima utembelee kinyozi angaa mara tatu kwa wiki ili kuhakikisha si kichaka.
Pia, lazima dume liwe tayari kwenda ‘waxing’ angalau mara mbili kwa mwezi, kuhakikisha kwamba hizo nywele za sehemu nyeti zinashughulikiwa vilivyo.
Mojawapo ya harufu zinazonikera zaidi ni ile ya jasho. Kama unataka unase jicho langu, lazima uwekeze kwa kununua viondoa harufu vya viwango vya kimataifa.
Bidhaa hii unapaswa kujipaka kila baada ya kuoga kuhakikisha kwamba huna kutuzi kwapani. Mbali na viondoa harufu, lazima pia uwekeze katika marashi ili kila unapopita karibu nami au hata kunikumbatia huniachii uvundo.
Ndiposa ikiwa unataka kunichumbia, lazima uwe tayari kubeba begi kila uendapo; mkoba utakaokusaidia kuhifadhi hivi vitu vyote. Kwa kila kaka anayekubali kuwa mchumba wangu, hii ndio huwa zawadi ya kwanza kutoka kwangu”.