Makala

MWANASIASA NGANGARI: Kiongozi aliyetimua Jaramogi kupitia Kongamano la Limuru

June 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na KYEB

JEREMIAH Joseph Mwaniki Nyagah anakumbukwa kama mwanasiasa aliyestaafu kutoka katika ulingo wa siasa na kwenda kuishi maisha ya kawaida kijijini licha ya kuhudumu na kutia fora katika wizara za Kilimo na Elimu.

Nyagah alizaliwa kijijini Igari, Embu, mnamo Novemba 24, 1920 na alianza elimu yake katika shule ya msingi ya Kimishenari ya Anglikana katika eneo la Kabare (Kaunti ya Kirinyaga) mnamo 1925.

Baadaye, alihamishiwa Kagumo, Nyeri, ambapo alifanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance mnamo 1937 (nambari ya usajili 427) na kisha kujiunga na Chuo cha Makerere, Uganda, mnamo 1940 kusomea diploma kwa miaka mitatu.

Nyagah alikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kufanya Mtihani wa Cheti katika Shule ya Cambridge nchini Kenya.

Miongoni mwa watu maarufu aliosoma nao katika Shule ya Alliance ni B.M. Gecaga (ambaye baadaye walifunza naye katika shule ya Kahuhia, Murang’a, ambapo mwanasiasa mtajika Kenneth Matiba alikuwa mwanafunzi wao) na Njonjo.

Kutoka Makerere, Nyagah alirejea nchini Kenya mnamo Januari, 1944, na kuwa mwalimu. Kati ya 1944 na 1958, Nyagah alifundisha katika shule mbalimbali na vyuo. Alikuwa mwalimu wa kwanza wa Shule ya Kangaru, Embu iliyokuwa na wanafunzi 30 pekee.

Alipoteuliwa kuwa waziri wa Elimu, Nyagah alitumia fursa hiyo kuzuru kila kona ya eneo la Kati ambapo alitangamana na wakazi na viongozi wa makanisa haswa Kanisa la Anglikana.

Kabla ya uteuzi wake kuwa afisa wa elimu katika eneo la Kiambu, Nyagah alijiendeleza kimasomo katika Chuo Kikuu cha Oxford ambapo alisomea elimu kati ya 1952 na 1954.

Wakati huo, kundi la Mau Mau lilikuwa likiendeleza harakati zake za kutaka kukomboa nchi kutoka mikononi mwa wakoloni.

Mnamo 1957, serikali ya wakoloni ilitangaza uchaguzi ufanyike Machi 1957 ili kuruhusu kundi la kwanza la Waafrika wanane kujiunga na bunge (Legco).

Alipoteza uchaguzi baada ya kubwagwa na mwalimu aliyesomea Afrika Kusini, Bernard Mate, aliyepata asilimia 51 ya kura huku Nyagah akipata asimilia 12.

Wengine waliokuwa wakiwania kiti hicho ni Eliud Mathu, mbunge wa kwanza Mwafrika katika Legco, wakili David Waruhiu na Stephen Kioni, Katibu Mkuu wa kwanza wa Chama cha Walimu (KNUT).

Bunge la Legco

Katika bunge la Legco, wawakilishi wanane wa Waafrika wakiongozwa na Tom Mboya walishinikiza viti vingine sita vitengewe Waafrika.

Shinikizo zilisababisha Allan Lennox-Boyd, waziri wa nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Waingereza, kuleta katiba mpya mnamo 1957 ambapo alitengea Waafrika viti zaidi.

Nyagah aliwania ubunge katika eneobunge jipya la Embu mnamo 1958 na akaibuka mshindi.

Kabla ya kujitosa katika siasa, Nyagah aliporejea kutoka chuoni Oxford aliteuliwa kuwa naibu afisa wa elimu wa Kiambu.

Nyagah alihusika katika kuhakikisha kuwa shule za jamii ya Wakikuyu zinafundishwa mtaala wa serikali.

Serikali ya wakoloni ilikuwa imefunga shule hizo kutokana na kigezo kwamba zilikuwa zikishirikiana na vuguvugu la Mau Mau, Jomo Kenyatta na viongozi wa chama cha KAU.

Shule hizo zilishutumiwa kwa kutoa mafunzo ya uchochezi dhidi ya serikali ya wakoloni.

Nyagah alikuwa miongoni mwa wanaharakati wa kwanza wa kutetea masilahi ya wafanyakazi. Aliwahi kuhudumu kama Katibu wa Chama cha Watumishi wa Serikali, tawi la Kiambu.

Alikutana na Mboya, mpiganiaji mkuu wa haki za wafanyakazi na mwanasiasa, katika afisi za chama wa wafanyakazi mtaani Kariokor, Nairobi.

Lakini mchango wake katika chama cha skauti kilimzolea sifa tele kimataifa.

Nyagah alijiunga na chama cha maskauti alipokuwa akisoma katika Shule ya Upili ya Alliance mnamo 1937.

Alisaidia chama cha maskauti kutovunjiliwa mbali na serikali ya wakoloni kutokana na madai kwamba kilishirikiana na vuguvugu za kupigania uhuru.

Baada ya Kenya kujipatia uhuru wake, Nyagah aliboresha zaidi chama cha maskauti huku akitumia methali: Udongo upate uli maji.

Alisema kuwa ilikuwa kupitia chama hicho ambapo vijana waliweza kupewa mafunzo yafaayo.

Baadaye aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Chama cha Maskauti nchini Kenya.

Alipokuwa Chuoni Oxford mnamo 1950, alitawazwa kuwa Mfalme wa Maskauti.

Mnamo Februari, 1982, Nyagah alitunukiwa medali ya juu zaidi katika chama cha maskauti. Alitunukiwa medali ya Bronze Wolf kutokana na mchango wake mkubwa kwa chama hicho kimataifa.

Hadi kufikia wakati alipoaga dunia alitambuliwa na kuheshimika kama baba wa chama cha maskauti Kenya.

Nyagah alikuwa na ushawishi mkubwa kisiasa miongoni mwa jamii ya Wambeere wa eneo zima la Embu.

Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Legco, aliteuliwa kuwa naibu spika wa kwanza Mwafrika. Jukumu lake la kwanza lilikuwa kumwapisha Kenyatta kuwa mbunge wa Kigumo katika ukumbi wa Fort Hall (katika Kaunti ya Murang’a) baada ya Kenyatta kuachiliwa huru kutoka kizuizini.

Lengo lilikuwa kumwezesha Kenyatta kujiunga na Legco na baadaye kuongoza viongozi wa Kanu katika kongamano la Lancaster jijini London mnamo 1961.

Nyagah alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria kongamano hilo. Aliteuliwa kuwa naibu waziri katika wizara ya Kawi mara baada ya Kenya kujipatia uhuru wake mnamo 1963.

Alihudumu katika wizara mbalimbali kati ya 1966 na 1992.

Mnamo 1964, Nyagah alikuwa miongoni mwa viongozi wachache walioenda Amerika kusomea taaluma ya uongozi.

Aliporejea aliteuliwa naibu waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi chini ya Daniel arap Moi huku mwanafunzi wake wa zamani Kenneth Matiba akihudumu kama Katibu wa Wizara.

Mnamo 1966, Rais Kenyatta alimteua Nyagah waziri wa Elimu, wadhifa alioshikilia kwa miaka mitatu.

Kabla ya uteuzi wake, Wizara ya Elimu iliyokuwa ikiongozwa na Joseph Otiende, ilikuwa na misukosuko chama cha Knut kilipoongoza maandamano mara tatu kikitaka kubuniwa kwa tume ya kuajiri walimu.

Mnamo Novemba 1966, Nyagah aliwasilisha bungeni mswada wa kutaka kubuniwa kwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC). Mswada huo wa TSC ulipitishwa na bunge mnamo 1966 na tume iliundwa na kuanza kutekeleza majukumu yake mnamo Julai 1, 1967.

Tume ya TSC ilitwikwa jukumu la kuajiri walimu wote katika shule za umma.

Nyagah alipunguza vyuo vya kutoa mafunzo ya ualimu hadi 16 na akageuza vyuo vilivyoathiriwa kuwa shule za upili.

Nyagah alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliokutana katika Baa ya Corner mnamo 1966 chini ya uongozi wa Ronald Ngala. Wengine waliohudhuria mkutano huo ni G.G. Kariuki, Clement Lubembe, Makone Ombesa, John Okwanyo na Justus ole Tipis.

Ni katika mkutano huo ambapo waliunda njama ya kummaliza kisiasa Makamu wa Rais Jaramogi Odinga. Ni katika kikao hicho ambapo waliandaa kongamano la Limuru mnamo Machi 1966 ambapo Odinga alitimuliwa kutoka wadhifa wake.

Katika kongamano la Limuru Nyagah aliteuliwa kuwa mmoja wa manaibu wanane wa rais.

Mnamo 1969, Nyagah alihamishiwa katika wizara ya Kilimo kuchukua mahali pa McKenzie aliyeamua kustaafu kutokana na sababu za kiafya.

Nyagah alisaidia pakubwa katika kuhakikisha kuwa kilimo kinasalia uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya. Sekta ya kilimo kilichangia asilimia 25 ya mapato ya Kenya.

Alijipata pabaya kufuatia uhaba wa mahindi nchini mnamo 1978 alipodaiwa kuuzia Msumbiji mahindi na kuacha maghala ya kuhifadhi nafaka yakiwa matupu.

Wakati huo, Kenyatta alikuwa ameaga dunia na Moi amechukua hatamu za uongozi.

Baada ya uchaguzi wa 1979, wizara ya Kilimo iligawanywa mara mbili. Nyagah aliteuliwa kuwa waziri wa Maendeleo ya Mifugo.

Baadaye alihudumu katika wizara mbalimbali kama vile Maji, Habari na Mazingira.

Hatimaye, Nyagah alistaafu kutoka kwenye siasa mnamo 1992 wakati kulikuwa na mjadala mkali kuhusu mfumo wa vyama vingi.

Mwanawe Norman Nyagah, alimrithi baba yake na kuwa mbunge wa Gachoka kupitia chama cha Democratic chake Kibaki.

Mbali na Norman, Nyagah ana watoto wengine; Joseph, Mary Khimulu, Nahashon.

Bi Khimulu ni balozi wa Kenya katika shirika la Umoja wa Mataifa la Unesco. Nahashon ni mwenyekiti wa Tatu City. Nahashon amewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya kwa miaka miwili hadi 2003.

Mke wa Nyagah, Eunice Wambeere, aliaga dunia mnamo Oktoba 29, 2006. Nyagah alifariki mnamo April 10, 2008, katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Nairobi akiwa na umri wa miaka 88.

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke