• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Alianza kwa kuuza chupi lakini sasa ni mmiliki wa kampuni

Alianza kwa kuuza chupi lakini sasa ni mmiliki wa kampuni

NA MWANGI MUIRURI

MWAKA wa 2003, Bi Wamucii Kinyari alikuwa mchuuzi wa soksi na chupi za wanaume katika jiji la Nairobi, biashara aliyoanza kwa mtaji wa Sh500.

Alikuwa amehitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Upili ya Kariti, Kaunti ya Nyeri mwaka wa 2002 na mwito wake wa kitaaluma ulikuwa uandishi wa habari.

“Hata hivyo, babangu alikataa katakata niingie taasisi ya uandishi habari akinitetesha kuwa hiyo haikuwa kazi ya watu walio na maono makubwa kuhusu maisha yao,” anasema.

Huku akiwa hana lingine la kutumainia maishani mwake, alianza kusaka marafiki zake waliokuwa wamehamia Nairobi na akajiunga nao huku akitafuta mbinu ya kujisukuma kimaisha.

Baada ya kusaka nafasi za kazi na kukosa, maisha yake yaligeuka kuwa ya mahangaiko lakini alipatana na jamaa wa kwao nyumbani aliyemsaidia kwa kumpa Sh500.

“Nilifanya hesabu ya haraka nikaona pesa hizo zingenisaidia pakubwa ikiwa ningeziingiza kwa biashara. Niliamua kununua soksi na chupi za kiume kwa kuwa nilikuwa na ufahamu kuwa mwanamke huwa na nafasi bora zaidi ya kuuzia wanaume bidhaa hizo,” asema.

Asema faida yake kwa siku ilikuwa ni Sh100 ambazo zilimsaidia kujisukuma kimaisha huku akingojea nafasi nyingine bora ya kujitafutia riziki.

Hata hivyo, dhuluma za askari wa jiji za kumkamata mara kwa mara na kumpokonya bidhaa zake zilimsukuma nje ya uchuuzi na akajipata akiwa kibarua katika hoteli ya mabanda, kazi yake ikiwa ya kuosha vyombo.

“Mshahara wangu wa kazi hiyo ya hoteli ulikuwa Sh100 kwa siku ambapo nilikuwa naingia kazini saa 12 asubuhi na kuondoka saa tatu usiku.

“Nilitegemea usaidizi wa mamangu kunisaidia kulipa nyumba huku mshahara wangu ukinijalia tu kulipa nauli ya kufika na kutoka kazini,” asema.

Kwa miaka miwili mtawalia alijisukuma katika hoteli hiyo lakini akaanza kuingiwa na wasiwasi kuhusu maisha yake ya mbeleni.

“Mwaka wa 2005 ulikuwa unaingia na ndipo nikajipa maazimio ya mwaka mpya. Nilipiga magoti saa sita kamili ya mkesha wa mwaka mpya na nikamsihi Mungu anijalie mema maishani kwa kuwa nilikuwa na uhakika hakuniumba niishi maisha ya kibarua,” asema.

Anasema kuwa aliamua kuwekeza ndani ya imani ya Ukristo ambapo alitarajia mema ya kumfanikisha kimaisha.

“Hatua hiyo ya kumpa Mungu kipao mbele katika maisha yangu ya umasikini mkuu ilinisaidia kuanza kuwa na mtazamo wa matumaini katika maisha yangu. Ilinisaidia pakubwa kuanza kuwa mtulivu nikingoja siku yangu ya Baraka. Utulivu huo ndani ya imani ulianza kujiangaza usoni mwangu na hata nikaanza kuongeza uzani licha ya umasikini wangu,” asema.

Bi Wamucii akikagua hesabu za mauzo alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali. Picha/ Mwangi Muiruri

Na hatimaye mwenge wa imani yake ulijitokeza mwaka wa 2006 ambapo kampuni ya kutengeneza sabuni ya Geisha ilizindua kampeni za kusaka warembo wa kuisaidia katika mauzo.

“Nilidokezewa na rafiki yangu kuhusu nafasi hiyo na nikatuma maombi ya kupewa kazi hiyo. Kulihitajika warembo 10 na nikachukuliwa,” asema.

Alijituma katika kazi hiyo na katika mwezi mmoja, alikuwa amefanikiwa kuuza masabuni hayo kwa kiwango mara 20 dhidi ya wenzake wote tisa pamoja.

“Ni katika harakati hizo ambapo sauti yangu ilitumika katika matangazo ya kibiashara ya sabuni ya Geisha ambapo niligutushwa na mashabiki wangu kuwa sauti yangu pia inenifaa katika safu ya muziki,” asema. Mwaka wa 2011, alizindua kanda yake mpya ya nyimbo za injili ambapo alielezea masaibu yake ya kimaisha katika ngoma – Mbona moyo wangu wahuzunika?

Kanda hiyo ilimfaa sana kimapato kwa kuwa, chini ya miezi mitatu, alikuwa amejipatia faida ya Sh100, 000.

“Niliimarika kiroho kwa kuwa nilifahamu imani yangu kwa Mungu ndiyo ilikuwa inazawadiwa. Mimi nilibakia tu kumshukuru Mungu huku nikijua nilitarajia makuu kutoka kwake,” asema.

Mwaka wa 2012, huku akiwa na kanda tatu za muziki ambazo zilikuwa zikifanya vyema, alipata kazi katika kitengo cha mauzo katika kituo cha Redio cha Kameme FM, kwa sasa kikiwa chini ya milki ya kampuni ya Mediamax.

Hapo ndipo alipata mtaji wa kutosha wa kujipanua kiriziki ambapo alizindua kampuni yake ya kuratibu sherehe mbalimbali, ushauri wa mauzo na pia kurekodi kanda zake za kimuziki.

Kwa mwezi, jumla ya mapato yake huwa ni ya kuridhisha kwake kwa kuwa halalamiki kuandamwa na jinamizi la shida tele zinazowakumba wengi wa Wakenya maishani kufuatia umasikini wa kusikitisha.

Ili kujiongezea mianya ya kupanua maisha yake, ashajiunga na Chuo kikuu cha Nairobi ambapo anatarajia kupata shahada ya sanaa.

Huku akiwa na miaka 34 kwa sasa, anashauri wote walio chini waige mfano wake wa imani kwa Maulana, waliofanikiwa wanyenyekee na wawe na moyo wa kusaidia walio chini na hatimaye wote wawe na subira katika maisha yao wakingoja Mungu awajalie neema zake.

“Mimi nimekuja kuelewa kuwa hakuna maisha duni kiasi cha kukupotezea matumaini. Mungu yuko nasi katika kila majaribio. Kaza imani yako na utarajie mema tu katika maisha. Hepa misukumo ya kujidunisha hata ukidunishwa na wengine na zaidi ya yote, tuliza roho yako ndani ya imani,” asema.

Bi Kinyari anasema kuwa bado hajachoka kumtumainia Mungu katika kuzidisha mapato yake na miaka 10 ijayo, ako na uhakika kuwa atakuwa bwanyenye mtajika wa kike sio tu kutoka kaunti yake ya kuzaliwa ya Nyeri, na kitaifa.

You can share this post!

Boca Junior FC inavyokuza vipaji mashinani

Askofu amuonya Uhuru dhidi ya kumsaliti Ruto 2022

adminleo