Tikiti ya Joho na Matiang'i yaibua hisia mseto Kilifi
Na CHARLES LWANGA
WABUNGE wa Kaunti ya Kilifi wametofautiana kuhusu kiongozi wa Pwani anayestahili kuwania urais katika uchaguzi wa 2022 kati ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi.
Wakati baadhi ya wabunge wanapigia debe azma ya Bw Joho, wengine wao wamekashifu hatua hiyo wakidai wanaompigia Bw Joho debe ni wasaliti.
Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya alidai wabunge ambao wanapeana uaminifu wao kwa kaunti nyingine badala ya kaunti zao ni wasaliti kwa Kaunti ya Kilifi.
Mbunge wa Kilifi Kusini, Bw Ken Chonga ni miongoni mwa wanaompigia debe Bw Joho wakisema ndiye kiongozi shupavu wa pwani na kumtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuwa mgombea mwenza wake.
Akizungumza huko Gede katika mkutano wa hadhara ya kuandaa bajeti ya Kaunti, alisema Kilifi itajiamulia yenyewe mgombeaji wa urais katika uchaguzi wa 2022.
Haya yanajiri wakati Gavana Kingi ameanza ziara za kuunganisha wakazi wa pwani kabla ya kutangaza azma yake hadharani ya kuania urais, hatua ambayo imeona akitofautiana kimaoni na Gavana Joho.
Bw Baya alishangaa ni kwa nini wabunge wengine hawawezi kukaa na watu wao badala ya kwenda Mombasa kuhudhuria sherehe za Eid ambapo walimpigia debe Bw Matiang’i kuwa naibu wa Bw Joho katika uchaguzi wa 2022.
“Kuketi na Bw Matiangi na kumwambia awe mgombeaji mwenza wa Bw Joho ni jambo la ushenzi. Zile nyakati za kusifu na kupigia viongozi makofi zilipita,” alisema.
Wabunge wengine ambao wangali waaminifu kwa Gavana Kingi ni Mbunge wa Magarini Michael Kingi, Bi Aisha Jumwa (Malindi), Bw Paul Katana (Kaloleni), Seneta Stewart Madzayo na mwakilishi wa wanawake Gertrude Mbeyu.
Wakati wa sherehe za Eid Ul-Fitr, Bw Chonga alisema Rais Uhuru Kenyatta tayari ameshaonyesha imani yake kwa Dkt Matiang’i kwa kumpatia baadhi ya majukumu yake ya kusimamia wizara zote serikalini.
“Nakwambia ndugu yangu Sultani, tunapokupatia jukumu la kuwa rais wa jamuhuri ya Kenya, hakikisha naibu wako awe Bw Matiang’i kwa sababu ana uwezo. Tumemjaribu na tunaona ana uwezo,” alisema.
Lakini Bw Baya alimkashifu na kusema viongozi wangetumia wakati huo na Dkt Matiang’i kutafuta suluhisho la dhuluma za mashamba eneo la Kilifi.
“Badala amwambie kuhusiana na kufurushwa kiholela kwa wakazi eneo la Kilifi Kusini, unamwambia jinsi anafaa kuwa naibu rais. Pia mimi nilikuwa nimeitwa kuhudhuria baraza hilo lakini sikuenda. Kwa nini kiongozi aende kwa mwaliko wa Bw Joho badala ya kuwa mwaminifu kwa kiongozi wake wa Kilifi?” akasema.
Wabunge ambao wamekuwa wanaambatana na kupigia debe azma ya urais ya Bw Joho ni Bw Chonga, mbunge wa Ganze Teddy Mwambire na mwenzake wa Rabai William Kamoti.