Makala

Dawa na teknolojia huchangia maradhi ya zinaa – Watafiti

June 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ELIZABETH MERAB

DAWA za kisasa na teknolojia za mawasiliano zinahofiwa kuchangia kwa usambazaji wa magonjwa mengi zaidi ya zinaa.

Wataalamu wa afya wanasema dawa ya Pre-exposure Prophylaxis, almaarufu kama PrEP ya kuzuia uambukizaji wa HIV inayosababisha Ukimwi, pamoja na ueneaji wa mitandao ya kijamii zimefanya watu wengi kuwa wazinifu na hivyo basi kutojali kushiriki mapenzi kiholela.

Ingawa hakujakuwa na uchunguzi wa kitaalamu kutoa takwimu halisi za ueneaji wa magonjwa ya zinaa kwa njia hizi, wataalamu wanashuku ongezeko la magonjwa hayo ni kwa sababu ya masuala hayo.

Wiki iliyopita, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilitoa ripoti iliyosema kwamba watu zaidi ya milioni moja wenye miaka kati ya 15 na 49 ulimwenguni huambukizwa magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kuepukika.

Hii ni kumaanisha kwamba kila siku kuna mtu mmoja kati ya 25 ambaye huambukizwa magonjwa hayo yanayojumuisha kaswende, kisonono miongoni mwa mengine.

Ingawa lengo la PrEP lilikuwa ni kuepusha watu wasio na HIV ambao wako kwenye uhusiano wa kimapenzi na walioambukizwa wasishikwe na ugonjwa huo, dawa hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya hasa na vijana wanaoshiriki ngono kiholela.

Hali hii imesababisha hofu kwa wataalamu wa afya kwani dawa hiyo haiwezi kuepusha uambukizaji wa magonjwa mengine ya zinaa, ilhali wanaoitegemea huwa hawajali kutumia mbinu nyingine za kujiepusha na madhara kama vile utumiaji wa mipira ya kondomu.

Mbali na haya, Prof Matilu Mwau ambaye ni mtaalamu katika Shirika la Utafiti wa Kimatibabu nchini Kenya (KEMRI), anasema mitandao ya kijamii pia imesemekana kufanya iwe rahisi kwa watu kupata wapenzi wengi kwa wakati mmoja.

“Nadhani suala kubwa linaloibuka ni ikiwa watu wameacha kutumia kondomu. Watu wanasahau kwamba PrEP si dawa inayozuia magonjwa yote na vilevile, dawa za kupunguza makali ya HIV (ARV) hazistahili kutumiwa kuzuia magonjwa ya zinaa,” akasema Prof Mwau.

Mtaalamu wa utafiti katika Kaunti ya Kilifi, Dkt Simon Masha alisema kuwa kumekuwepo ongezeko kubwa la magonjwa ya zinaa miongoni mwa watu wanaotumia PrEP, na huenda kutotumia kondomu kunasababisha idadi hiyo kuongezeka.

Serikali iliruhusu utumizi wa dawa hiyo katika mwaka wa 2015 miongoni mwa watu walio hatarini kuambukizwa HIV lakini baadaye dawa hiyo ikaanza kupatikana katika soko huru.

Kulingana na Dkt Jordan Kyongo ambaye ni mtafiti wa masuala ya afya ya umma, watu takriban 46,000 walianza kutumia PrEP mwaka uliopita.

“Tunachofahamu ni kwamba kuna ongezeko la watu wanaotumia PrEP na kupuuza mbinu nyingine za kujilinda kutokana na magonjwa ya zinaa kama vile utumiaji wa kondomu,” akasema Dkt Kyongo.

Kinachotia hatari zaidi ni kuwa baadhi ya magonjwa hayo kama vile kisonono na kaswende, yamekuwa sugu katika miaka ya hivi majuzi na kuwa vigumu kutibiwa.

Magonjwa haya huweza kusababisha wanaume na wanawake kukosa uwezo wa kupata watoto, na kwa wanawake, yanaweza kufanya watoto kufa wakiwa tumboni kabla ya kuzaliwa.