• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:55 AM
FKF yatangaza mipango ya Stars dhidi ya DR Congo

FKF yatangaza mipango ya Stars dhidi ya DR Congo

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imetangaza mipango yake ya mechi ya pili na mwisho ya kirafiki kabla ya Kombe la Afrika (AFCON) dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itakayosakatwa jijini Madrid nchini Uhispania hapo Juni 15.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limesema Jumatatu kwamba vijana wa Sebastien Migne watatoka kambini jijini Paris nchini Ufaransa mapema Juni 15 kuelekea Madrid. Ni safari ya ndege ya saa moja na dakika 55 hivi.

Mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) watamenyana na DR Congo saa moja usiku siku hiyo na kulala jijini Madrid kabla ya kurejea kambini Juni 16.

Kenya, ambayo ilishiriki AFCON mara ya mwisho mwaka 2004, itafunga safari ya kuelekea Misri mnamo Juni 19. Itakuwa na siku tano pekee za kuzoea hali ya anga ya Misri ambayo ni joto wakati huu tofauti na kibaridi kinachopatikana nchini Ufaransa.

Wakenya wanatarajiwa kufahamu kikosi chao cha mwisho cha wachezaji 23 Jumatatu (saa moja usiku) kutoka kwa orodha ya 27 ambao wamekuwa wakishiriki kambi ya mazoezi jijini Paris.

Katika mechi zingine za kirafiki za kujiandalia kwa AFCON zilizosakatwa Jumapili, mabingwa watetezi Indomitable Lions ya Cameroon walilemea Chipolopolo ya Zambia 2-1 mjini Majadahonda nchini Uhispania, DR Congo ikalazimishiwa sare tasa dhidi ya Burkina Faso mjini Marbella nchini Uhispania, Uganda ikaandikisha 0-0 dhidi ya Turkmenistan mjini Abu Dhabi nchini Milki za Kiarabu nayo Ghana ikaduwazwa 1-0 na Namibia mjini Dubai katika Milki za Kiarabu.

Mnamo Jumamosi, Angola ilicharaza Guinea-Bissau 2-0 mjini Penafiel nchini Ureno nayo Zimbabwe ikatoka 0-0 dhidi ya wenyeji Nigeria mjini Asaba.

Kenya ilicheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki Juni 7 ikilemea Madagascar 1-0 jijini Paris nchini Ufaransa.

Tunisia na Ivory Coast pia zilikuwa uwanjani siku hiyo ambapo zilipepeta Iraq 2-0 na Comoros 3-1, mtawalia. Mechi moja ambayo Kenya itakuwa makini kupata ufahamu wake ni ile inayokutanisha Algeria na Burundi, leo.

Kenya itakutana na wapinzani hawa wawili katika AFCON na mechi ya kufuzu kushiriki soka ya wachezaji wanaocheza katika mataifa yao almaarufu CHAN, mtawalia.

Algeria ikishinda Burundi pembamba ama ipige sare ama kuchapwa, itaipa Kenya matumaini inaweza kukabiliana nayo vilivyo katika mechi yake ya ufunguzi ya Kundi C hapo Juni 23.

Vijana wa Migne pia watakutana na Senegal na Tanzania katika mechi za makundi jijini Cairo. Kabla ya mashindano kuanza, Algeria pia itapimana nguvu na Mali hapo Juni 16, nayo Senegal ivaane na Nigeria siku hiyo. Tanzania itachuana na Misri katika mechi ya kirafiki mnamo Juni 13.

Makala ya mwaka 2019 yanaleta pamoja mataifa 24 ambayo yamegawanywa katika makundi sita ya timu nne nne.

Timu mbili za kwanza katika kila kundi zitaingia raundi ya 16-bora pamoja na timu nne zitakazokamilisha mechi za makundi katika nafasi ya tatu zikiwa na alama nyingi.

Kenya, ambayo imeshiriki AFCON mwaka 1972, 1988, 1990, 1992 na 2004, inatumai kuandikisha historia yake kwa kupita mechi za makundi katika makala haya ya 32.

You can share this post!

Kahawa Queens yaibuka moto wa kuotea mbali

Mashtaka ya uchochezi dhidi ya Kuria yafutwa

adminleo