• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Dereva ndani miaka 15 kwa kumuua mpenziwe

Dereva ndani miaka 15 kwa kumuua mpenziwe

Na RICHARD MUNGUTI

Mahakama Kuu Jumatatu ilimhukumu dereva wa matatu miaka 15 gerezani kwa kumuua mpenziwe katika mtaa wa Buruburu miaka saba iliyopita.

Jaji Stellah Mutuku alisema Omari Waithaka anastahili kuadhibiwa kwa vile alitamatisha maisha ya msichana aliyekuwa anatumainiwa na familia yake.

“Maisha ni ya thamani kuu na kamwe haipasi kutamatishwa kiholela na mtu yeyote,” alisema Jaji Mutuku.

Jaji huyo alisema mshtakiwa alitenda uhalifu huo baada ya kuzozana na mpenziwe.

Jaji Mutuku alimpata Omari na hatia ya kumuua mpenziwe baada kuukaribisha mwaka mpya kwa kubugia pombe na kutafuna miraa usiku kucha.

Omari Waithaka alimtupa Yvonne Njoki Maina kutoka orofa ya pili baada ya kumkaba koo na hatimaye akamdunga kisu kisha “ akamtosa kutoka orofani.”

Jaji Stellah Mutuku alimweleza mshtakiwa, “Ulijawa na wivu uliposikia Njoki akizugumza na mwanaume aliyetambuliwa kwa jina Wambugu. Ulimtesa Njoki kabla ya kumuua kinyama na kupeleka mwili wake hospitali ya Metropolitan kudanganya amejirusha kutoka orofa ya pili.”

Akasema Jaji Mutuku,“Hii mahakama imekupata na hatia ya kumuua Yvonne Njoki Maina mnamo Januari 1 2012. Upande wa mashtaka umethibitisha kweli kweli ni wewe ulimuua mpenzi wako,” Jaji Stellah Mutuku alimweleza dereva wa matatu Omari Waithaka.

Omari alitenda uhalifu huo mtaani Jericho Nairobi mnamo Januari 1, 2012.

Wapenzi hao walikuwa wakisherehekea shamra shamra za kuukaribisha mwaka mpya wivu ulipomshika Omari baada ya kusikia Njoki akizugumza na mwanaume mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja Wambugu.

Jaji Stellah Mutuku aliyempata Omari na hatia ya kumuua Njoki alisema , “mshtakiwa alitamatisha maisha ya binti huyo kwa kumdunga na kisu kisha akamrusha kutoka orofa ya pili kuficha kitendo chake.”

Jaji Mutuku alisema kuwa mshtakiwa alivurugana na marehemu kwa muda hata akawapigia wazazi wake na mshtakiwa akampokonya simu.

“Baba ya marehemu alimsikia akipiga duru kwa simu akiomba msaada kwa vile Omari alikuwa anataka kumuua,” Alisema Jaji Mutuku.

Alisema mshtakiwa alimshinda nguvu Njoki kwa kumkaba koo hadi akazirai kisha akamdunga na kisu mikononi na tumboni.

“Damu ilitapakaa chumbani na katika sehemu alipoanguka Njoki,” akasema Jaji Mutuku.

Mahakama hiyo ilisema mshtakiwa alikuwa amepanga kumuua Njoki kwa vile alikuwa amemchumbia mwanaume mwingine.

“Njoki alikuwa amechoka kudhulumiwa na mshtakiwa. Siku Omari aliyomuua mpenziwe alimchukua kutoka nyumbani kwa wazaziwe mtaani Lang’ata Nairobi. Walienda kubugia pombe Nairobi West kisha wakateremka hadi mtaani Jericho kuukaribisha mwaka mpya,” alisema Jaji Mutuku akisoma uamuzi wake.

Baada ya kumrusha kutoka orofani mshtakiwa alimchukua Njoki kwa gari lake la matatu na kumpeleka Hospitali ya Metropolitan.

Wakili Karathe Wandugi alisema atakata rufaa kupinga adhabu hiyo.

You can share this post!

Mashtaka ya uchochezi dhidi ya Kuria yafutwa

Raia wa Pakistan kizimbani baada ya kunaswa na mali ya Sh75m

adminleo