Bodaboda na abiria waliopata ajali walipiwa gharama za matibabu Kiambu
Na LAWRENCE ONGARO
WAHUDUMU wa bodaboda wapatao 55 waliopata ajali watanufaika kutokana na ufadhili wa fedha ambazo zilitolewa na Kaunti ya Kiambu.
Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu, alisema Jumatatu tayari serikali yake imetoa Sh6 milioni zitakazotumika kulipia huduma za matibabu na vifaa vyote vinavyohitajika katika matibabu ya wahudumu hao wa bodaboda.
“Baadhi ya wale walioletwa katika hospitali ya Thika Level 5 na ile ya Kiambu Level 5 wamekaa hapa kwa zaidi ya miezi miwili na hawana jinsi ya kupata matibabu kwa sababu ya kukosa fedha,” alisema Bw Waititu.
Aliyasema alipozuru hospitali ya Thika Level 5 ambapo aliamuru wahudumu hao watibiwe halafu serikali ya Kiambu ilipie gharama hizo yote.
Dkt David Ndegwa anayewatibu wagonjwa wa mifupa katika hospitali ya Thika Level 5, alisema ni jambo la kusifiwa kwa sababu walioathirika watapokea matibabu ya haraka na chini ya siku nne hivi wataweza kujitembeza wakitumia mikongojo.
“Hospitali imelazimika kununua vifaa muhimu vinavyohitajika ili kufanikisha mpango huo. Sasa tutafanya upasuaji wa dharura na kuona ya kwamba mgonjwa anapata nafuu haraka iwezekanavyo,” alisema Dkt Ndegwa.
Alizidi kueleza ya kwamba wahudumu wengi wa bodaboda hushindwa kugharimia matibabu yao kwa sababu vifaa vinavyohitajika kwa upasuaji ni vya bei ya juu mno.
Avunjika mguu
Bw James Waithaka, ambaye alianguka akiwa kwa pikipiki eneo la Murang’a, akiwa ni abiria alisema alivunjika mguu wa kulia lakini anazidi kupata nafuu kwa mwezi mmoja ambao umepita.
Baadhi ya walioahirika na kupata majeraha mabaya wameshukuru hatua ya Gavana Waititu, wakisema wanatumai kurejea makwao hivi karibuni wakiwa wamepata nafuu.
Charles Ng’ang’a, aliyepata ajali ya bodaboda miezi miwili iliyopita anasema juhudi za Gavana Waititu kuwalipia gharama zote za hospitali ni hatua nzuri inayostahili kupongezwa.
“Mimi binafsi ninashukuru sana kwa Gavana Waititu kutulipia gharama za hospitali na kwa sasa tuna matumaini ya kufanyiwa upasuaji wa haraka ili tupate nafuu haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Alex Kimani aliyeonekana na maumivu mengi miguuni mwake.
Mwingine aliyepata majeraha mabaya ya mguu wa kulia ni James Waithaka anayesema ajali yake ilitendeka mwezi mmoja uliyopita mjini Murang’a.
“Nilikuwa katika bodaboda na nilipokuwa nikipiga kona fulani nilipogongana na lori lililonitupa kichakani. Baadaye nilijipata katika hospitali ya Thika Level 5,” alisema Bw Waithaka.