Habari

Mwanafunzi wa chuo kikuu akamatwa kwa kuingia Ikulu kinyume cha sheria

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PSCU

MWANAFUNZI wa chuo kikuu anayesomea taaluma ya uhandisi amekamatwa kwa kuingia Ikulu kinyume cha sheria.

Brian Kibet Bera, 25, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) alikamatwa na polisi kwa kuingia Ikulu ya Nairobi kinyume cha sheria.

Mwanafunzi huyo, ambaye alikwea lango moja la Ikulu, alipigwa risasi na polisi wanaopiga doria kwenye lango hilo baada ya kuchomoa kisu alipoagizwa asimame.

Tukio hilo lilisababisha yeye kuumia katika bega la kushoto.

Kisa hicho kilitokea Jumatatu saa kumi na dakika tano jioni na mshukiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa na kusajiliwa katika Kitabu cha Matukio nambari 39 kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu.

Uchunguzi waendelea

Uchunguzi unaendelea kubainisha nia yake ya kuingia Ikulu kinyume cha sheria na hatua zifaazo zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Taarifa kutoka Ikulu inakumbusha umma kwamba Ikulu ni pahala palipotengwa kuwa chini ya ulinzi mkali kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo Yanayolindwa (Protected Areas Act).

Kwa sababu hiyo, hakuna yeyote anaruhusiwa kuingia Ikulu pasipo na ruhusa kutoka kwa asasi ama maafisa waliotwikwa mamlaka jukumu hilo.