• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
UFUGAJI: Ndege wa umaridadi wamemuinua kimapato

UFUGAJI: Ndege wa umaridadi wamemuinua kimapato

Na SAMMY WAWERU

LENGO la kufuga ndege wa umaridadi lilikuwa kurembesha boma lake, na  hatima yake itaishia kuwa kitega uchumi.

Bi Margaret Njeri Maina, anafuga ndege hao chini ya mradi wake wa kuku, Gratia Poultry, ulioko mita chache kutoka Chuo Kikuu cha Wanawake cha Kiriri, Kaunti ya Kiambu.

“Nilipania kurembesha mazingira ya boma langu kwa ndege ambao ni maridadi,” anadokeza Bi Njeri.

Mradi huo, Gratia Poultry, umesitiriwa na kipande cha ardhi chenye ukubwa wa futi 50 kwa 80.

Aidha, umegawanywa kwa sehemu kadhaa hususan kuhifadhi vifaranga anaototoa kwa kiangulio, kuku waliokomaa na ndege.

Kizimba cha nyuni wake kilichoundwa kwa mbao, nyaya na mabati, kimechukua nafasi ya futi 20 kwa 15.

Ndicho makazi ya kanga, bata mzinga (turkey) na batabukini (goose wingi geese).

Njeri pia anafuga bata wa majini (mallards) na njiwa. Kizimba kimegawanywa ili kusitiri kila aina ya nyuni, huku vifaranga wakiwa na makazi yao maalumu.

Kuanza biashara

Bi Njeri 36, alianza ufugaji wa kuku mwaka wa 2016. “Ni kupitia ziara nilizofanya kwa wafugaji wakati nikitafiti kuanzisha mradi wa kuku ndipo nikagundua ndege ni rahisi mno kufuga, pamoja na gharama yao kuwa ya chini,” anaelezea.

Anasimulia kuwa aling’oa nanga na bata bukini wawili, walioanguliwa kutoka kwa mayai matano aliyonunua.

Kila yai aliuziwa Sh200 na anasema kwamba aliyanunua kutoka kwa wafugaji tofauti ili kuepuka kuwazalisha kutoka kwa ‘familia’ moja (inbreeding), suala linalofanya ndege kuwa dhaifu.

“Batabukini walifuatwa na batamzinga mwaka wa 2017, ambapo nilinunua watano kila mmoja nikiuziwa Sh2, 000,” anasema Bi Njeri ambaye ni mama wa watoto wawili.

Anaendelea kueleza kwamba alichinja mmoja na kugundua nyama ya bata mzinga ni tamu sana na yenye ladha ya kipekee.

Ni kufuatia hilo, mfugaji huyu na familia yake walisherehekea wawili zaidi, na kusalia na wawili, wa jinsia ya kike na kiume ili kuwazalisha.

“Hii leo ukizuru mikahawa inayopika nyama za ndege wanaoliwa, uagize ya bata mzinga utajua thamani yake. Ni ghali mno,” anasema.

Bata wa majini, ambao ni maridadi kimaumbile kwa kuwa na kichwa cha rangi ya kijani, manyoya ya zambarau, kahawia au kijivu na kanga-ndege wanaomuingizia pesa kama njugu, aliwanunua mwaka uliopita, 2018.

Mfugaji huyu anafichua kwamba alinunua bata wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike, kila mmoja akigharimu Sh2, 000.

Pia, kutoka kwa wafugaji tofauti, alinunua kanga wawili wa kike na mmoja wa kike, wote akiuziwa jumla ya Sh2, 400. Njiwa aliwaleta baadaye mwaka uliopita, japo anasema furaha yake ni kuona wakipaa na kutua.

Biashara yenye faida tele

Mradi huo umenawiri kutoka wazo la kurembesha boma hadi biashara inayomuingizia maelfu ya pesa, mbali na kutegemea uanguaji wa vifaranga wa kuku.

“Kabla kuanzisha ufugaji, nilikuwa nimewekeza katika biashara ya kuchora na kuchapisha (design & printing). Nilipoona shughuli za ufugaji zina mapato, nilisitisha kazi hiyo, ili kuuvalia njuga kikamilifu,” Njeri anasema.

Ana viangulio vitatu, cha kutotoa mayai 2112, 1056 na 500.

Kwa wiki, huangua vifaranga wa kuku wasiopungua 6, 000 na ni kupitia biashara hiyo wateja wake wameinua kwa kiasi kikubwa ufugaji wa ndege.

“Wateja wa vifaranga wa kuku ndio walewale wanaonunua ndege ninaofuga. Wanapokuja, hufurahishwa na mandhari yaliyotwaliwa na rangi maridadi ya ndege na kelele zao zinazohinikiza mazingira na kuyafanya yavutie. Huagiza ndege hata kabla watage na kuanguliwa,” anafafanua.

Wakati wa mahojiano alisema huwa hauzi mayai ila huyazalisha vifaranga (value addition).

“Uuzaji wa vifaranga una faida kuliko mayai,” anasema.

Huangua vifaranga kwa viangulio anavyotumia katika kuku. Alisema huuza vifaranga wa ndege walio na umri wa kati ya siku moja hadi wiki moja. Wanaopitisha umri huo, huwahifadhi ili kuimarisha jitihada zake.

Idadi ya ndege

Kwa sasa ana batamzinga tisa wa kike na wawili wa kiume. Kanga, ni jumla ya saba – wawili wakiwa wa kiume. Idadi ndogo ya kanga inatokana na soko lake ambalo ni mithili ya mahamri moto sokoni.

Bata bukini ni 12, wawili wakiwa wa kiume. Bata wa majini ni 10 wa kike na 5 wa kiume.

Ana njiwa zaidi ya 15. Wakati wa mahojiano tulipata akiwa na vifaranga 10 wa ndege anaofuga, na alisema wote wana oda na hata kulipiwa ada.

Alifichua kwamba siku kadhaa zilizopita, alileta ndege wawili wanaojulikana kama vulturine guinea fowl, aina ya kanga maridadi na machachari.

Kwa mujibu wa takwimu za mfugaji huyu, batabukini hutaga wastani wa mayai 20 kwa mwezi. Anapoyaangua kwa viangulio, kifaranga wa siku moja hadi wiki moja humuuza Sh500.

Ingawa hajaweza kuibuka na mkondo sambamba wa utagaji wa kanga, Njeri anasema ndege hawa hutaga sana msimu wa baridi na ule ya wastani ikilinganishwa na wakati wa joto.

“Ni ndege wa mwituni, ambao wakiachiliwa hutaga popote. Nilishangaa kuona hutagia mchangani na kuficha mayai. Kuyapata huwa vigumu iwapo mkulima hatawafuatilia kwa umakinifu wa hali ya juu.

“Kinyume na bata bukini na bata wa majini, ambao ni watulivu, wanaotafuta mahala maalum pa kutagia na kusalia hapo, kanga wanahitaji kuongozwa. Hata hivyo, kanga ndio ndege nambari moja katika mauzo yangu,” anaelezea mfugaji huyu.

Anadokeza kuwa, kwa mwezi kanga mmoja hutaga zaidi ya mayai 15 huku kifaranga mmoja akigharimu zaidi ya Sh1, 000.

Batabukini, ndege watulivu na wanaoandamana pamoja kila wakati, utagaji wake si wa kuridhisha vile kwani kwa mwaka hutaga kati ya mayai 20 hadi 40.

Bi Margaret Njeri Maina akiwa na ndege anaofuga nyumbani. Picha/ Margaret Maina

Hata hivyo, ni ndege bora katika uatamiaji wa mayai na kutunza vikembe wake, ingawa Njeri huyaangua vifaranga kwa vifungulio.

Mbali na bata mzinga ambao hujiatamia mayai yake na kuangua vifaranga, mayai ya wale ndege wengine huyaangua kwa mashine (viangulio).

Bw Okuta Ngura, mtaalamu wa masuala ya ufugaji wa kuku na ndege, anasema maganda ya batamzinga ni magumu mno na yanawahitaji wenyewe kuyaatamia.

“Batamzinga wa kike husaidiana na wa kiume kuyaatamia,” anasema Bw Ngura ambaye hutoa huduma za kuku na ndege nchini na ukanda wa Afrika Mashariki kupitia kampuni yake ya Ngura Poultry Care.

Kwa mwaka, bata mzinga hutaga karibu mayai 100.

Kifaranga wa ndege huyu, Bi Njeri humuuza zaidi ya Sh1,000.

Uanguaji wa mayai ya ndege wengi huchukua muda wa kati ya siku 21 hadi 30.

Ndege wa umaridadi waliokomaa hununuliwa kwa pea, kiume na kike. Bata wa majini na kanga, pea moja hugharimu takriban Sh5, 000, huku bata bukini na mzinga ikigharimu Sh10, 000. Hukomaa miezi mitano baada ya kuanguliwa.

Lishe na changamoto

Njeri anasema ndege wanaofugwa tu kwa ajili ya umaridadi ni miongoni mwa nyuni rahisi zaidi kufuga;na biashara yenye faida ya haraka.

Kando na kuwalisha chakula maalumu cha kuku, na ambacho ni bei ghali, mfugaji huyu hupunguza gharama kwa kuwapa masalia ya chakula cha binadamu.

“Wanapenda ugali, punje za mchele na masalia mengine ya chakula. Pia, wanapenda majani kama ya mboga,” asema.

Wataalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji wanapendekeza ndege na kuku walishwe chakula chenye madini kamilifu.

“Vifaranga walishwe chick mash, wanaokua growers na wanaotaga layers mash,” anashauri Bw Okuta Ngura ambaye ni mtaalamu.

Mdau huyu, pia anahimiza umuhimu wa kuwanywesha maji mengi na safi.

Kulingana na Njeri, ndege anaofuga ni nadra kuathiriwa na magonjwa.

Bw Ngura hata hivyo, anasema magonjwa yanayoshuhudiwa kwa ndege ni kama vile; yanayoathiri sehemu za kupumua, kwa Kiingereza Chronic Respiratory Disease (CRD), Coccidiosis na Coryza.

Magonjwa mengine ni Newcastle na Salmonella.

Muhimu ni kwamba magonjwa hayo yanahitaji chanjo na matibabu.

Vimelea ni; viroboto, kupe, mchwa na minyoo.

Ili kuwadhibiti, Bi Njeri hudumisha kiwango cha juu cha usafi katika vizimba vya ndege na kuku, na hata katika mazingira.

Kando na kupulizia dawa dhidi ya vimelea, humwaga maji sakafuni na ukutani, ili kuwafurusha.

Mfugaji anashauriwa kuondoa ndege au kuku kizimbani wakati wa kupulizia dawa ya vimelea.

Njeri anasema kuwa, akiondoa gharama ya leba, chakula na matibabu, ndege hao humpa zaidi ya asilimia 50 ya mapato.

Ni muhimu kukumbusha kwamba ili kuruhusiwa kufuga ndege wa umaridadi na kurembesha boma, unapaswa kupata kibali kutoka kwa shirika la huduma ya wanyamapori nchini (KWS).

You can share this post!

Mwanafunzi wa chuo kikuu akamatwa kwa kuingia Ikulu kinyume...

WAKILISHA: Mchezo wa sarakasi wampaisha mtaani

adminleo