Habari Mseto

Ubadilishaji wa mitungi ya gesi wapigwa marufuku

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA ANITA CHEPKOECH

SERIKALI imepiga marufuku vituo vya gesi kujaza mitungi ya kampuni zingine.

Hii inamaanisha kuwa Wakenya hawataweza kubadilisha mitungi ya gesi ya kampuni tofauti na ile waliyo nayo jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Kawi (EPRA), Payel Oimeke, jana alisema hatua hiyo itasaidia kupambana na mitungi feki ya gesi na pia kuwahakikishia Wakenya wanaotumia gesi usalama wao.

Kujazwa kwa gesi mtungini kwa njia za haramu, kuundwa kwa mitungi feki inayofanana na ile ya kampuni asili ni baadhi ya sababu zilizochangia kuanzishwa kwa sheria hiyo.

“Kubadilishwa kwa mitungi ya gesi kiholela bila kuzingatia kampuni asili imekuwa ikiletea kampuni hizo hasara kubwa. Kampuni nyingi zimelazimika kuwekeza fedha katika kununua mitungi mingine iliyo salama kwa matumizi ya wateja wao kila mara kutokana na sokoni,” akasema Bw Oimeke.

Baada ya sheria hiyo kuanza kutekelezwa, EPRA sasa itahakikisha kwamba mitungu yote ambayo haijakaguliwa vizuri kabla ya kujazwa gesi na ina nembo zisizofaa imeondolewa.