• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
NGILA: Wakati wa wanawake kuvalia njuga teknolojia ni sasa!

NGILA: Wakati wa wanawake kuvalia njuga teknolojia ni sasa!

NA FAUSTINE NGILA

“Ni wakati wa kusema ukweli kuhusu sayansi ya maumbile. Uwezo wa mwanamke na mwanamume hutofautiana kutokana na sababu za kibayolojia, na tofauti hizi zimechangia pakubwa kwa asilimia ndogo ya wanawake katika sekta ya teknolojia.”

Usemi huu wa mhandisi wa kampuni ya Google, James Damore mnamo 2017, ulisababisha kutimuliwa kwake, aliposhikilia kuwa mapenzi ya wanawake kwa mahusiano yanapunguza uwezo wao katika teknolojia.

Hata hivyo, kutimuliwa kwake hakukubadilisha ukweli huu unaodhihirika katika kampuni nyingi za teknolojia nchini na kimataifa, ambapo asilimia ya wafanyakazi wanawake ni chini ya 30.

Na hili linatokana na hali kwamba wakati idara za nguvukazi zinatangaza ajira za nafasi za teknolojia, wanaume wengi kuliko wanawake hujitokeza.

Ni wazi kuwa duniani kote, kozi kama Sayansi ya Kompyuta na Teknolojia ya Mawasiliano huvutia wanafunzi wengi wa kiume kuliko wa kike.

Hali hii huishia kuwaathiri wasichana na wanawake kwa jumla, kwani wahandisi wanaounda programu za kompyuta kwenye kampuni hizo huishia kuziwekea sifa za kiume, na kusahau kuwa zitatumiwa na watu wa jinsia zote mbili.

Hivyo, tunafaa kuwafundisha wasichana wetu kuanzia wakiwa wa umri mdogo umuhimu wa teknolojia, ili waweze kufurahia na kuenzi uwezo wa kompyuta, na hatimaye kupigania nafasi ya wanawake katika teknolojia.

Utafiti umeonyesha kuwa wanaume wanawapiku wanawake kwa asilimia 12 kote ulimwenguni kwa matumizi ya intaneti, takwimu ambayo inaashiria kuwa bado wanawake hawako tayari kukabili wanaume kupunguza pengo hili katika taaluma ya teknolojia.

Na si hilo pekee. Katika uvumbuzi wa programu tajika humu nchini, zaidi ya asilimia 70 ya programu zinazozinduliwa zimeundwa na wanaume.

Kwenye vyuo vya teknolojia kama Moringa, wanafunzi wengi ni wavulana. Katika uanahabari, ni waandishi na watangazaji wanaume ambao wameshamiri katika ulingo wa kuripoti habari na makala ya teknolojia.

Huwezi kusema kuwa serikali imechangia katika pengo hili. Wanawake wanafaa kuvalia njuga teknolojia, hasa uvumbuzi unaosaidia kutatua changamoto zinazowakumba kama ukeketaji, ndoa za mapema, dhuluma za kimapenzi na muhimu zaidi, usawa wa kijinsia.

Jukumu hili likiachiwa wanaume litakuwa mzigo mkubwa kwa sababu ni vigumu wanaume kujiweka kwenye fikra za kike na kuunda programu za kuwakomboa dada zetu.

Hivyo, ili wasiachwe nyuma, wanawake wanafaa kutambua kuwa dunia ya sasa inaendeshwa kwa kasi ya teknolojia, na wakati wao wa kuchangia kwa maendeleo ya wanadamu ni sasa. Usawa huu wa kiteknolojia utasaidia kuleta usawa wa kijamii.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Tusipuuze kisa cha kijana kuingia Ikulu

WASONGA: Rotich atangaze mikakati ya chakula cha kutosha

adminleo