• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
AFYA: Hofu tele kampuni za unga kutotii maagizo

AFYA: Hofu tele kampuni za unga kutotii maagizo

Na PHYLLIS MUSASIA

WIZARA ya Afya imeonya kuwa kampuni za unga zisizofuata sheria ya kuongeza madini muhimu kwenye bidhaa zake kabla ya kuwauzia raia, zinaiweka nchi kwenye hatari ya kugharamia hasara ya mamilioni ya pesa kuhusiana na madhara ya kiafya yanayosababishwa na ukosefu wa madini hayo.

Wizara hiyo ilisema ukosefu wa madini kama vile vitamini A, B3, miongoni mwa madini mengine kwenye baadhi ya vyakula umesababaisha afya duni haswa kwa maisha ya akina mama wajawazito na watoto.

Akizungumza kwenye mkutano uliowaleta pamoja washikadau wa kampuni za unga kutoka Magharibi, Nyanza na Bonde la Ufa, mwakilishi kutoka wizara ya Afya Bw John Mwai aliomba serikali iingilie kati na kuhakikisha kuwa wenye kampuni hizi wanazingatia matakwa yote yanayohusiana na sheria za kupakia bidhaa kabla ya kuziuza.

“Kuongeza madini kwenye bidhaa kama vile unga wa ugali, unga wa ngano, mafuta ya kupikia na chumvi ni jambo muhimu sana kwa sababu ni njia moja ya kuwasaidia wananchi kuishi maisha bora. Inatupasa sisi sote tuwe makini wakati tunapoandaa bidhaa zetu na kabla ya kupakia kwenye mifuko tofauti ni sharti tuwe tumeongeza madini kama ilivyo kisheria,” akasema Bw Mwai.

Kupuuzilia mbali sheria hizo, Bw Mwai alionya, kunamaanisha kuwa nchi iko katika hatari ya kukadiria hasara ifikapo kila mwisho wa mwaka.

Alitoa mfano kwa nchi ambazo zinaendelea kukua huku akisema kuwa ukosefu wa madini katika vyakula umesababisha nchi hizo kukadiria hasara ya hadi asilimia tano maarufu ‘GDP’ kila mwaka. Hii, alisema inalinganishwa na shilingi bilioni 20 hadi 30 za marekani.

Profesa Daniel Sila kutoka katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknologia cha Jomo Kenyatta ambaye pia alihudhuria mkutano huo alisema takwimu mpya zilizorekodiwa baada ya utafiti kufanywa na chuo hicho zinaonyesha kwamba nusu ya idadi ya kampuni ambazo zinahusika kutengeneza unga nchini hazizingatii suala la kuongeza madini kwenye unga.

“Takribani asilimia 70 ya unga ambao unatumiwa na Wakenya kwenye miji mikuu huwa umefikia kiwango hitajika ikilinganishwa na asimilia 24 ya unga ambao unatumika katika maeneo ya mashambani na mitaa duni,” akaeleza Profesa Sila.

Utafiti aidha ulionyesha kuwa thuluthi moja ya idadi ya watoto wanaozaliwa katika maeneo ya mashambani na mitaa ya mabanda huwa katika hatari kubwa ya kuathiriwa na magonjwa kama vile upofu ambao hutokea wakati mama akiwa mjamzito.

“Mara nyingi unapata kuwa kule mashambani watu wengi wanatumia unga wa kusaga na kwa hivyo kunakuwa na uwezekano mwingi wa kukosa madini muhimu. Jambo hili ni changamoto kubwa ambayo serikali inapaswa kujua jinsi ya kueneza ujumbe mashinani kuhusiana na umuhimu wa madini haya,” akasema.

Changamoto kama vile ukosefu wa ufahamu wa teknologia, ukosefu wa mashine, bei ghali ya madini ni baadhi ya mambo ambayo yalitajwa kurudisha nyuma sekta ya unga haswa kwa wale wenye kampuni ndogondogo.

Ili kustawisha miundo msingi kwenye sekta hiyo, wizara ya afya kwa ushirikiano na chuo kikuu cha JKUAT imekuwa ikieneza umuhimu wa madini kwenye vyakula kupitia ratiba inayofadhiliwa na Muungano wa Ulaya nchini.

You can share this post!

WASONGA: Rotich atangaze mikakati ya chakula cha kutosha

Ashtakiwa kujiunga na Al-Shabaab, ISIS na ISIL

adminleo