TAHARIRI: Mazungumzo ni hatua nzuri ya kukuza utaifa
Na MHARIRI
ALIPOAPISHWA mnamo Novemba 2017 katika uwanja wa michezo wa Kasarani kwa muhula wa pili, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuwaita viongozi wa upinzani na kujadiliana kuhusu mwelekeo wa kuchukua kama nchi.
Kauli yake ilitokana na mgawanyiko mkubwa uliopo hadi sasa, ambao chanzo chake ni kususiwa kwa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017.
Tungetaka kusifu Rais Kenyatta kwa kutimiza ahadi yake na kukutana na kinara wa NASA Raila Odinga, lakini tusisitize umuhimu wa kuhusishwa kwa viongozi wengine, haswa katika upinzani.
Tayari vinara wenza katika upinzani wametaja hatua ya Bw Odinga kukutana na rais peke yake kama usaliti wa kisiasa.
Japo mkutano wa rais na Bw Odinga umewapa wengi matumaini ya kutuliza joto la kisiasa nchini, ni vyema kutopuuza mchango wa vinara wenza katika upinzani Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula.
Madhumuni ya kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga yawe kuunganisha Wakenya wote na wala si jamii au familia mbili.
Kilele cha joto la kisiasa kilikuwa hafla ya kumwapisha Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi,’ jambo ambalo lilivutia macho ya ulimwengu mzima.
Ukweli mchungu ni kuwa, Wakenya wamegawanyika katika makundi mawili. Kuna kundi linaloamini kuwa Rais Kenyatta ndiye kiongozi aliyechaguliwa na kuapishwa, kwa mujibu wa katiba. Kwa upande mwingine, wafuasi wa Bw Odinga nao wanasikiza tu kauli ya upinzani.
Uasi wa aina hii si mzuri kwa nchi. Ikiwa tunataka kuendelea mbele, na serikali ifanikiwe katika nguzo zake nne za maendeleo ilizojiwekea, basi lazima kuwe na mandhari tulivu ya kisiasa.
Ni matumaini yetu kuwa mkutano wa viongozi hao wawili ni mwanzo wa kulainisha siasa zetu kabla ya uchaguzi wa 2022.
Kando na wanasiasa, rais anapaswa kuwaita wadau wengine kufanya mazungumzo kuhusiana na masuala ibuka kutokana na uchaguzi uliopita, ili kukomesha hali ya wasiwasi na Kenya isonge mbele.
Mazungumzo ya kijamii pia yanafaa kutekelezwa kwa lengo la kukuza umoja, utangamano na amani miongoni mwa Wakenya.