• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
GWIJI WA WIKI: Abed Wambua

GWIJI WA WIKI: Abed Wambua

Na CHRIS ADUNGO

UFANISI katika chochote unachokifanya ni zao la kujiamini.

Kujiamini ni mwanzo bora katika kulijaribu jambo lolote duniani.

Huwezi kabisa kufanikisha kikao na nyangumi iwapo wewe mwenywe unayaogopa maji ya bahari.

Usikate tamaa wala kuongozwa na pupa ya kutaka kufaulu kwa siku moja. Jifunze kuvuta subira ili nayo ikujalie heri.

Thamani ya mwalimu huboreshwa na wanafunzi wake.

Ukubwa wa thamani hiyo ambayo hutarajiwa kuwa kiini cha sifa zake, hushinda ubora wa pesa na vitu vyote vingine vya msimu!

Pania sana kutenda wema siku zote kwa sababu hifadhi ya jina zuri katika fikra za wanafunzi wako ndiyo malipo bora zaidi ambayo mwalimu hupata.

Upeo wa mafanikio ya mtu hutegemea pakubwa juhudi zake binafsi, nidhamu na imani aliyonayo kuhusu jambo.

Mungu alipokuumba, alikupa kipaji, uwezo wa kukitumia vyema kipawa hicho na jukwaa la kuwadhihirishia walimwengu talanta yenyewe.

Huu ndio ushauri wa Bw Abed Musomba Wambua – mtunzi mahiri wa mashairi na kocha wa tenisi ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Muthale Girls, Kaunti ya Kitui.

Mwalimu Wambua anaamini kwamba hakuna kitu kinachoridhisha zaidi nafsi ya mwenye kutenda jambo kuliko kuwafanyia watu kazi nzuri itakayodumu katika kumbukumbu zao kutokana na jinsi itakavyoyaathiri maisha yao na mikondo ya fikra zao.

Maisha ya awali

Wambua alizaliwa mnamo 1985 viungani mwa mji wa Kitui akiwa kitindamimba katika familia ya watoto saba wa marehemu Bi Mary Njeri na Bw Meshack Wambua.

Baada ya kusomea katika chekechea ya Majengo Nursery, Kitui alijiunga na Shule ya Msingi ya Muslim, Kitui mnamo 1992.

Ni huko ndiko alikoufanyia mtihani wake wa KCPE mwishoni mwa 2000.

Alama nzuri alizozipata zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Ikanga Boys, Kitui mnamo 2001 na akahitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) shuleni humo mwishoni mwa 2004.

Anatambua ukubwa wa mchango wa walimu wake wa awali katika kumwelekeza vilivyo, kumshauri ipasavyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Aliyemshajiisha zaidi kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni Mwalimu Waziri.

Anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake ya dhati kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa na kuhamasishwa pakubwa na Bw Kamuti aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili.

Isitoshe, Kamuti ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika shule mojawapo katika Kaunti ya Kitui, alimwelekeza vilivyo kuandika Insha bora zilizomzolea tuzo za haiba kubwa.

Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili alaa kulihali.

Mbali na marehemu Bi Liguyani, mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Profesa Aswani Bulibo wa Chuo Kikuu cha Laikipia.

Mtihani mgumu zaidi ambao Wambua alikabiliana nao baada ya kukamilisha KCSE ni vita vya ndani ya nafsi vilivyompa msukumo wa kutaka kuwa mwanasheria au kujitosa kikamilifu katika ulingo wa Kiswahili na kuwa ama mwalimu mashuhuri, mwandishi maarufu au mtunzi shupavu wa mashairi.

Uanasheria na ualimu ni taaluma ambazo Wambua alizitamani sana tangu utotoni mwake.

Ingawa hivyo, watoto wengi wa hirimu yake walikosa kabisa kuona thamani ya ndoto hizo za mwenzao kwa wakati huo.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Wambua kwa sasa katika Kiswahili unatokana na tukio la yeye kufundishwa na wasomi ambao mbali na kubobea ajabu kitaaluma, pia waliipenda na kutawaliwa na ghera ya kuipigia chapuo lugha hiyo.

Usomi

Mnamo 2006, alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, Bewa la Laikipia, kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Historia).

Anaungama kuwa motisha zaidi ya kukisomea Kiswahili ilitoka kwa wanafunzi wenzake waliokuwa wakimpongeza kwa matamshi fasaha, umilisi wake wa lugha na upekee wa kiwango chake cha ubunifu katika utunzi wa mashairi.

Msukumo wa kutaka kujiendeleza kitaaluma ni miongoni mwa mambo ambayo kwa sasa yanamchochea kutaka kurejea chuoni kusomea Shahada ya Uzamili katika Isimu ya Kiswahili.

Ualimu

Baada ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa la Laikipia) mnamo 2010, Wambua alianza kufundisha Kiswahili na somo la Historia katika Shule ya Upili ya Ikanga. Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mnamo Machi 2011, alijiunga na Shule ya Upili ya Muthale Girls, Kitui baada ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kumwajiri kwa kandarasi.

Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa zaidi kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi ambao walianza kushiriki mashindano mbalimbali ya tamasha za muziki na drama hadi kufikia kiwango cha kitaifa.

Isitoshe, aliteuliwa kuwa Mwalimu Msimamizi wa somo la Historia na kocha wa mchezo wa tenisi shuleni humo. Ilikuwa hadi Oktoba 2011 ambapo TSC ilimwajiri kabisa, kisha kumdumisha Muthale Girls chini ya Mwalimu Mkuu Bi Veronica Waweru.

Anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea pakubwa mtazamo wake kwa masomo anayofundishwa na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Lugha shuleni Muthale Girls, ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mara matokeo ya KCSE yanapotolewa.

Tangu 2015, Wambua amekuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi ya Pili ya Kiswahili (Sarufi na Matumizi ya Lugha). Uzoefu huo umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Uandishi

Wambua anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Nyingi za Insha na mashairi aliyoyatunga yalimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa mwenzake.

Aidha, ufundi mkubwa katika tungo alizozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanika katika ulingo wa Kiswahili.

Mapenzi ya kutunga mashairi na kuyaghani mbele ya hadhira ni fani iliyojikuza ndani yake tangu akiwa tineja.

Amekuwa akitunga mashairi mengi kwa minajili ya tamasha za kitaifa za muziki. Anaendelea kwa sasa kuchapisha diwani ambayo anaamini itabadilisha pakubwa sura ya kufundishwa kwa somo la Ushairi miongoni mwa walimu na wanafunzi wengi katika shule za upili za humu nchini.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri wa chuo kikuu, Wambua anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Miongoni mwao Bi Lavenda Claire aliyeyoyomea Amerika kusomea uanasheria baada ya kufaulu vyema katika mtihani wa KCSE 2012.

Wengine ni Bi Charity Muingo na Bi Lilian Patience waliotawaliwa na mapenzi ya dhati kwa Kiswahili.

Wambua anatambua pia upekee wa mchango mkewe Bi Nancy Muluki katika kumhimiza pakubwa kukichapukia.

Kwa pamoja, wamejaliwa watoto wawili: Meshack na Mary. Pia wanamlea kijana yatima Onesmus Kithome ambaye kwa sasa ni mwanafunzi katika chuo cha mafunzo anuwai.

You can share this post!

Achanganyikiwa kortini kung’amua pingu alizokiri...

KAULI YA WALIBORA: Ustaarabu, kwa baadhi ya watu, ni...

adminleo