Michezo

Migne akiri jeraha la Mandela ni pigo kubwa Harambee

June 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Sebestien Migne amekiri kwamba jeraha litakalomkosesha beki Brian Mandela fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mwezi huu nchini Misri ni pigo kubwa kwa kikosi chake cha Harambee Stars.

Mandela ambaye huchezea Maritzburg United ya Afrika Kusini aliumia goti mnamo Jumatatu akishiriki mazoezi na wenzake jijini Paris, Ufaransa.

Nyota huyo pia hatakuwa sehemu ya kikosi cha Stars kitakachochuana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi ya kupimana nguvu itakayosakatwa jijini Madrid, Uhispania mnamo Juni 15.

“Mandela ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika safu ya nyuma ya Stars. Hatakuwa sehemu ya kikosi kitakchopeperusha bendera ya Kenya nchini Misri. Itabidi sasa kutafuta suluhu ya haraka,” akatanguliza Migne.

“Habari hizi si nzuri kwa Stars na kwa Mandela mwenyewe. Musa Mohamed ambaye ni beki wetu mwingine wa haiba kubwa, alipata jeraha wakati wa mchuano wa kirafiki dhidi ya Madagascar. Itakuwa hatari kumchezesha dhidi ya DR Congo, japo tutamtegemea sana nchini Misri,” akasema.

“Stars waliwashinda Ghana katika mkondo wa kwanza wa michuano ya kufuzu kwa fainali za AFCON bila ya huduma za wachezaji wengi wa haiba. Hilo halistahili kutuaminisha kwamba mambo bado ni mazuri,” akaongeza Migne.

Kenya ambao wameratibiwa kutua Misri mnamo Juni 19, watafungua kampeni zao za Kundi C dhidi ya Algeria mnamo Juni 23.

Vijana wa Migne watachuana baadaye na Tanzania mnamo Juni 27 kabla ya kushuka dimbani kupimana ubabe na Senegal mnamo Julai 1.

Itakuwa ni mara ya nne kwa Stars kuvaana na kikosi cha Senegal almaarufu Lions of Teranga katika hatua ya makundi kwenye fainali za AFCON.

Vikosi hivyo vimewahi kukutana katika fainali za 1990, 1992 na 2004.

Uwanja wa 30 June

Mechi zote zitakazowakutanisha Stars na wapinzani wao katika Kundi C nchini Misri zitasakatwa uwanjani 30 June jijini Cairo.

Kulingana na mvamizi Michael Olunga, kikosi cha Stars kinatawaliwa na kiu ya kusajili ushindi katika nyingi za mechi zao ili kurejesha Kenya katika ramani ya soka ya Afrika.

Olunga ambaye kwa sasa huchezea Kashiwa Reysol ya Japan, alikuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Stars kilichowazamisha Madagascar kwa bao 1-0 katika mchuano wa kirafiki nchini Ufaransa mwishoni mwa wiki jana.

“Uchache wa mabao tuliyofungwa na wapinzani katika mechi za kufuzu kwa fainali hizi ni jambo la kutia moyo,” akasema Olunga.

Stars ambao walishiriki fainali za AFCON kwa mara ya mwisho 2004 nchini Tunisia, watakuwa na siku tano pekee za kuzoea joto jingi la Misri, tofauti na baridi kali inayoshuhudiwa kwa sasa nchini Ufaransa.

Makala ya mwaka 2019 yatakuwa ni mara ya sita Kenya kushiriki mashindano haya ambapo itakumbukwa ilicheza 1972, 1988, 1990, 1992 na mwaka 2004.

Hata hivyo, safari hizi tano za awali, Kenya haikuwahi kupita awamu ya makundi.