Habari Mseto

MKU yazindua kituo cha uzamifu na uzamili bewa la Nairobi

June 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimezindua kituo cha masomo ya uzamifu katika bewa la Nairobi kwa lengo la kuwapa wanafunzi nafasi kupiga hatua zaidi kimasomo.

Dkt Francis Njoroge ambaye ni mwanakamati katika chuo hicho alisema wataendelea kuzindua vituo vingine kama hivyo katika vitengo vingine vya Chuo hicho katika maeneo mengine.

Alisema kituo hicho kitakuwa cha kipekee na kisasa likiwa na vyumba tofauti vya kuendesha mikutano, na pia vya kufanyia mashauriano na wahadhiri.

“Tutahakikisha hata mwanafunzi aliye nchi za nje anaweza kuwasiliana na mhadhiri yeyote kwa mashauriano ya kuedesha maswala ya utafiti. Hii ni kutokana na vifaa vya hali ya juu vya kiteknolojia vilivyoko humo,” alisema Dkt Njoroge.

Alisema kituo hicho kitakuwa na maktaba ya kisasa ambayo kitakuwa kimehifadhi vitabu vya kisasa vya kusoma wakati wa kufanya utafiti, huku pia likiwa na vipakatalishi vitakavyotumiwa na wanafunzi.

Kulingana na Dkt Njoroge, kituo hicho kitakuwa na vyumba 100 tofauti vinavyoweza kutumika kwa semina, mikutano ya wahadhiri na wanafunzi, na vyumba vya wanafunzi kujifanyia mambo yao kwa utulivu.

Alitoa changamoto kwa vyuo vya kielimu kote nchini kuzingatia maswala ya utafiti na ubunifu miongoni mwa wanafunzi.

“Vyuo vikuu ambavyo havizingatii maswala ya utafiti na ubunifu katika vyuo vyao wanalinganishwa kama vyuo vya upili. Kwa hivyo, ni vyema kupiga hatua zaidi kimasomo,” alisema Dkt Njoroge.

Kujiongeza maarifa

Alisema mpango huo ni muhimu kwa sababu utawapa motisha wanafunzi kujizatiti na kujiongeza maarifa zaidi kupitia uzamifu.

Alizidi kueleza kuwa hiyo tu itafanikiwa mradi tu kuwe na ushirikiano mwema kati ya mhadhiri na mwanafunzi.

Alisema kituo hicho pia kitawafaa wanafunzi walio katika nchi za nje kwa sababu wataweza kufanya mawasiliano ya kidijitali kupitia mazungumzo ya kiteknolojia.

“Ikiwa mwanafunzi aliye nchi za nje angetaka kufanya utafiti wake kupitia maktaba hiyo katika kitengo cha Nairobi, anaweza kupata ufahamu wowote anaoutaka,” alisema Dkt Francis Njoroge.

Alisema wanafunzi kadha wameanza tayari kujiendeleza na masomo ya uzamifu kwa ushirikiano wa karibu na wahadhiri walioko huku wakifanyiwa maandalizi kamili.