• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mudavadi: Uongozi usitumike kuficha mafisadi

Mudavadi: Uongozi usitumike kuficha mafisadi

Na SAMMY WAWERU

VIONGOZI wa umma wanaotajwa kuhusishwa na visa vya ufisadi wanapaswa kujiuzulu mara moja.

Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi amesema kuendelea kwao kusalia mamlakani kunazuia asasi za kukabiliana na ufisadi kuendesha uchunguzi.

Bw Mudavadi ambaye amewahi kuhudumu kama makamu wa rais, waziri na naibu waziri mkuu katika serikali za awali alisema Jumanne washukiwa wa ufisadi wanaendelea kujificha uongozini na kuendelea kufuja mali ya umma.

Alisema watuhumiwa hawapaswi kusifiwa wala kupewa nafasi kuwania viti vya kisiasa au kuteuliwa tena katika nyadhifa serikalini. “Ukitajwa kushiriki ufisadi unapaswa kujiuzulu.

“Rais ana mamlaka kukuita, akueleze alikuteua na anaona kazi haifanyiki ipasavyo. Kinachofuata ni aidha ujiuzulu au akupige kalamu,” alisema Bw Mudavadi.

Alisema umewadia wakati vyama pinzani viungane na kukashifu kwa pamoja kukithiri kwa sakata za ufisadi serikalini. Alisema kujitosa katika siasa isitumiwe kama njia ya kukwepa tuhuma za ufisadi na hata kuvunja sheria.

“Iwapo wewe ni mgeni wa kila wakati kwa mkurugenzi wa upelelezi wa jinai (DCI) kwa nini usifunguliwe mashtaka? DCI George Kinoti haandalii watu kahawa ofisini mwake, hatua ichukuliwe kwa wahusika,” alisema mbunge huyu wa zamani Saboti.

 

Idara ya DCI inayoongozwa na George Kinoti, afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma chini ya Noordin Haji na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ndizo kisheria zilizotwikwa jukumu kukabiliana na ufisadi.

  • Tags

You can share this post!

Apigwa risasi akiingia Ikulu ‘kumuua’ Uhuru

Mike Kamau: Msusi ambaye wanawake Murang’a wanamsifia

adminleo