KAULI YA MATUNDURA: Mchango wa fasihi ya Kiswahili katika kuhifadhi matukio muhimu ya historia
Na BITUGI MATUNDURA
MWAKA 2002, mtaalamu wa Kiswahili na utamaduni pendwa – Prof Kimani Njogu – aliwashangaza wanataaluma wa Kiswahili wa Afrika ya Mashariki aliposimulia kisa cha profesa mmoja wa fasihi aliyedai kwamba hakuwa amepoteza chochote kwa kutosoma fasihi ya Kiswahili.
Akizungumza kwenye kongamano la Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA), Prof Njogu alieleza jinsi alivyojaribu kueleza profesa huyo kwamba alikuwa amepoteza mengi – kwa mfano mapinduzi ya Visiwani Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964, ambayo yamefumbatwa katika riwaya za Kiswahili.
“Kuna ustaarabu gani katika kutojua jambo?” akauliza Prof Njogu.
Prof Njogu amehakiki kwa kina jinsi fasihi ya Kiswahili imefumbata mapinduzi hayo ya visiwani Zanzibar katika kitabu chake, Uhakiki wa Riwaya za Visiwani Zanzibar (Nairobi University Press, 1997).
Katika makala haya, ninaangazia jinsi tungo nyingine za Kiswahili zimefumbata matukio mengine muhimu ya kihistoria yaliyowahi kutokea Afrika ya Mashariki.
Riwaya ya Peter Munuhe Kareithi – Kaburi Bila Msalaba ( East African Publishing House, 1969) ni mfano mzuri wa riwaya ya kihistoria.
Utungo wa fasihi wa kihistoria huwa ni nadithi ya kubuni unaosimulia matukio halisi ya zamani yaliyo na uzito wa kijamii. Matukio haya mara nyingi huwa ni yale ambayo huathiri historia na mkondo wa jamii au taifa husika.
Mpaka baina ya matukio ya tungo ya kihistoria na matukio halisi huwa ni yepi? Katika utungo wa kihistoria, matukio halisi na wahusika halisi huumbwa kisanaa.
Katika historia, matukio na watu huelezwa jinsi walivyokuwa au kuonekana.
Katika tungo ambazo viunzi vyao vimejikita katika historia, matukio makuu ya historia hutumiwa kama muktadha wa matendo ya hadithi ambayo ama huwa ya kweli au ya kubuni.
Tungo za Kiswahili ambazo zimetumia viunzi vya matukio halisi ya kihistoria ni pamoja na Kaburi Bila Msalaba (P.M.Kareithi), Kasri ya Mwinyi Fuad, Kuli na Haini (S.A.Shafi).
Aidha tuna tamthilia za Kinjeketile (E.Hussein), Mukwava wa Uhehe (M.M.Mulokozi), Sundiata (E.Mbogo), miongoni mwa tungo nyingine.
Katika riwaya ya Kaburi Bila Musalaba, Kareithi amafaulu kueleza bayana na kwa njia sahili vita vya kuikomboa Kenya kutokana na utawala dhalimu za wakoloni.
Vita hivi vilivyojulikana kama vita vya Maumau ni kumbukumbu ya mambo aliyoyashuhudia mwandishi wakati wa hali ya hatari kabla ya Kenya kujinyakulia uhuru.
Mwandishi anaitamatisha riwaya yake kwa taswira ya kuhuzunisha.
Anasema, “Hii ndiyo iliyokuwa mara ya mwisho kwa meja Blue kuona watu wake. Ilikuwa mara ya mwisho kuona nchi yake aliyoipigania kwa miaka miwili […] Meja Blue ambaye ndiye aliyekuwa mkuu wa magaidi huko pande za Mathera alihukumiwa kunyongwa.”
Anasema kuwa waliomwona kwa mara ya mwisho ni mahabusu wa Mau Mau waliokuwa jela ya Nyeri, kwani wao ndio walimzika. Lakini hakuna ajuaye kaburi lake liko wapi.
Mwisho huu unaibua taswira ya kuhuzunisha kuhusu wazalendo kama akina Dedan Kimathi – ambao licha ya kujitolea mhanga katika juhudi za kuikomboa Kenya, hakuna aliyeuthamini mchango wao. Anwani – ‘Kaburi Bila Msalaba’ inaibua fahiwa ya usaliti waliotendewa mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya kwa kumwaga damu na kupoteza maisha yao.
Juhudi hizo hakikutuzwa wala kutambuliwa kikamilifu na viongozi walioshika hatamu za uongozi pindi uhuru ulipojiri.
Mpaka sasa, kuna mashujaa wengi ambao ‘makaburi yao hayana misabala’ kwa misingi kwamba michango yao katika nchi zao haitambuliwi.
Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi katika Chuo Kikuu cha Chuka