• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Akasirisha hakimu kutaka dhamana ya Sh10,000 katika kashfa ya Sh300m

Akasirisha hakimu kutaka dhamana ya Sh10,000 katika kashfa ya Sh300m

Na Richard Munguti

MMOJA wa washukiwa 15 wa kashfa ya dhahabu ya Sh300 milioni alizomewa na hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Francis Andayi alipoomba apunguziwe dhamana hadi Sh10,000.

William Onyango Otieno, aliyekana kushiriki katika uuzaji wa dhahabu feki aliomba mahakama impunguzie dhamana kutoka Sh200,000 hadi Sh10,000.

“Nimetoka katika familia isiyo na ukwasi mkubwa kifedha. Jamaa sita wa familia yangu hawakufanikiwa kupata dhamana uliyoamuru ila wameweza tu kupata Sh10,000. Naomba uniachilie kwa kiwango hicho tu mheshimiwa,” Onyango alimsihi hakimu.

Lakini ombi hilo halikuchukuliwa kwa urahisi na Bw Andayi hata akamwuliza mshtakiwa, “kwani unanichezea akili. Unanipima akili. Nimekupunguzia dhamana hii mara kadha lakini sasa umerudi tena kortini kunipima akili iwapo naweza kukulegezea kamba.

“Umepunguziwa dhamana hii mara kadhaa na haukutosheka, sasa wataka nikupunguzie zaidi dhamana hadi Sh10,000. Huu ni mzaha sasa.”

Akijibu Onyango alisema, “Sikuchezei akili kamwe mheshimwa. Nimekueleza tu kile kinaweza kupatikana.”

Lakini kabla ya hakimu kutoa uamuzi, wakili Stanley Kang’ahi anayemwakilisha mshtakiwa pamoja na washukiwa wengine alimweleza hakimu , “usichukulie ombi hilo kwa uzito. Watu wa familia yake wako hapa kortini na tayari wako na dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu alizopewa hapo awali. Watamlipia. Hawakuwa wamewasiliana naye. Samahani.”

Onyango na washukiwa wengine wanadaiwa walifanya njama za kumlaghai mfanyabiashara Sounthorn Chanthavong Dola za Marekani 3 milioni (Sh300m) wakitumia ujanja.

Wanadaiwa mnamo Februari 8 na 25, 2019 jijini Nairobi, walimwonyesha Bw Chanthavong, mkurugenzi wa kampuni ya Simuong Group fito feki vya dhahabu na masanduku ya chuma wakidai yalikuwa yamepakiwa dhahabu wakijua ni uwongo.

Bw Otieno pamoja na Philip Aroko, Robert Ouko ajulikanaye pia kama Paul Ouko Owiti na Rickey Thomas Okoth almaarufu Tom Okot walikabiliwa na shtaka la kumlaghai Bw Chanthavonmgo dola za marekani 3 milioni (Sh300m) wakidai watamuuzia dhababu halisi.

Kesi hiyo itatajwa baada ya miezi miwili kuwezesha afisa anayeichunguza kupokea ushahidi wa kimitandao.

You can share this post!

Hapa majitapo tu kuelekea fainali za Chapa Dimba

Aliyenaswa na pingu akiwa mlevi asukumwa rumande

adminleo