• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sitaogopa kuwakamata wanasiasa wachochezi – Matiang’i

Sitaogopa kuwakamata wanasiasa wachochezi – Matiang’i

ERIC MATARA na GEOFFREY ONDIEKI

WAZIRI wa Usalama, Fred Matiang’i amewaonya wanasiasa wanaotoa matamishi ya uchochezi yanayolenga kuzua vurugu nchini kuwa watakamatwa.

Waziri Matiang’i, aliyekuwa akizungumza alipokuwa akizindua kituo cha kutoa paspoti cha Idara ya Uhamiaji mjini Nakuru, aliwataka maafisa wa usalama kutega masikio na kuwanasa watu wanaotoa matamshi ya kikabila ambayo huenda yakazua uhasama wa kikabila.

Dkt Matiang’i alisema serikali itakabiliana na watu wanaotoa matamshi ya uchochezi bila kujali vyeo vyao katika jamii.

“Serikali itawakamata viongozi haswa wanasiasa wanaotoa matamshi ya uchochezi. Viongozi wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kuendeleza umoja nchini na wala si kutoa matamshi ya kuwatenganisha raia. Kila Mkenya ana haki ya kuishi katika sehemu yoyote ya nchi,” akasema Dkt Matiang’i.

“Kuna watu wanaotoa matamshi ya uchochezi haswa katika eneo la Bonde la Ufa. Hakuna mtu aliye juu ya sheria kwa kuchochea watu kuzua vurugu,” akaongezea.

Dkt Matiang’i alitoa onyo hilo huku kukiwa na hali ya taharuki katika baadhi ya eneo la Bonde la Ufa haswa kaunti za Elgeyo Marakwet, Baringo, Pokot Magharibi na Laikipia ambako wezi wa mifugo wamekuwa wakivamia wakazi mara kwa mara.

Dkt Matiang’i alitoa onyo hilo mara baada ya kufanya kikao cha faragha na viongozi wa kidini na maafisa wa usalama wa Bonde la Ufa katika jumba la Menengai Social Hall mjini Nakuru.

Duru ziliambia Taifa Leo kuwa Dkt Matiang’i aliunga mkono operesheni inayoendelea ya kuwapokonya bunduki raia pamoja na maafisa wa Polisi wa Ziada (NPR).

You can share this post!

Babake aliyeingia Ikulu aililia serikali impe mwanawe...

Ngilu asimulia mahakamani alivyoponea kifo

adminleo