Ngilu asimulia mahakamani alivyoponea kifo
NA KITAVI MUTUA
GAVANA wa Kitui Charity Ngilu Jumatano alielezea Mahakama ya Kitui alivyoponyoka kifo kwa tundu la sindano 2016 wakati gari la zimamoto la kaunti lilipomkanyaga rafikiye marehemu Martha Mwangangi.
Bi Ngilu alitoa simulizi hiyo ya kuatua moyo mbele ya Jaji Lilian Mutende akisema matukio hayo ya Disemba 16, 2016 yatasalia akilini mwake milele, akifichua kwamba kifo cha Bi Mwangangi bado kinamhuzunisha hadi leo.
Gavana huyo alikuwa akitoa ushahidi kwenye kesi ambapo dereva wa gari hilo la zimamoto Philip Isika Tito ameshtakiwa kwa kumuua Bi Mwangangi.
Bi Ngilu alieleza kwamba alikuwa amealikwa kuwatuliza waandamanaji ambao vioski vyao vilibomolewa na serikali ya kaunti kwenye soko la Kalundu na baadaye kukatokea kisa hicho cha mauti.
“Mheshimiwa gari hilo halikuwa limebeba maji ya kuzima moto wala hakuwa na wazima moto ndani,” akasema Bi Ngilu akiongeza kwamba baada ya Bi Mwangangi kukanyagwa na dereva huyo aliendesha gari hilo kuelekea upande mwingine.