Hospitali ya kina mama kujifungua kuwafaa wengi mpakani Nakuru na Baringo
Na PHYLLIS MUSASIA
NI habari njema kwa wakazi wanaoishi katika vijiji vya mpaka baina ya Kaunti za Nakuru na Baringo baada ya kituo kipya na cha kwanza cha afya cha akina mama kujifungua kuidhinishwa katika kijiji cha Sarambei, kaunti ndogo ya Rongai.
Kituo hicho chenye vifaa muhimu vinavyohitajika kuligana na sheria na kanuni za idara ya afya nchini, kina takribani vitanda 12, sehemu maalumu ya kupumzikia akina mama baada ya kujifungua, wadi na mashine spesheli za kupima ujauzito, mashine za kupima dalili za saratani ya uzazi, matangi ya maji safi ya kunywa miongoni mwa vifaa vinginevyo.
Hospitali hiyo ilifunguliwa rasmi Jumatano na Waziri wa Afya katika kaunti ya Nakuru Bw Zakayo Kariuki Gichuki.
Kulingana na waziri Gichuki, visa vingi vya kuwapoteza akina mama na watoto wachanga pindi tu wanapozaliwa, vimekuwa vikishuhudiwa katika maeneo hayo ya mpakani; jambo ambalo ndilo kiini cha kujengwa kwa hospitali hiyo.
“Limekuwa ni jambo la aibu sana kila mara tunapokea habari kuwa akina mama na watoto wanazidi kufa kila uchao kutokana na matatizo ya kujifungua wakiwa nyumbani,” akasema Dkt Gichuki.
Aliongeza kuwa wengi wa wakazi hupata wakati mgumu kusafiri mbali kama vile kwenye hospitali ya rufaa ya Nakuru au ile ya Eldama Ravine ilioko Kaunti ta Baringo ili kupata matibabu lakini sasa ni afueni kwa akina mama wajawazito ambao sasa watanufaika na hospitali hiyo mpya.
Utafiti huo uliofanywa na shirikika moja la kimataifa umebaini kwamba, asilimia 56 ya akina mama nchini hujifungua wakiwa nyumbani huku asilimia 58 ikirekodiwa kwenye kaunti ya Nakuru kwa akina mama na watoto wanaoaga dunia wakati wa uzazi.
Na katika eneobunge la Rongai, Dkt Gichuki alisema asilimia 73 ya akina mama walisemekana kujifungua wakiwa nyumbani na kusaidiwa na wakunga wasiohitimu.
“Idadi hii ni kubwa mnamo na ya kutamausha. Mara nyingi tumejaribu sana kuwazia ni jinsi gani tunaweza kurudisha idadi hii chini na kuokoa maisha ya watoto na akina mama haswa wanaoishi vijijini na wakati huu tunaamini kila mmoja wenu atatumia nafasi hii ili kunufaika na hospitali hii,” akasema Dkt Kariuki.
Akina mama wenye umri wa kati ya miaka 19 hadi 49 ambao wana watoto wachanga wanahudhuria kliniki, pia walijumuishwa kwenye utafiti huo.
Aliwasihi wanaume wawe mstari wa mbele kuwahimiza wake zao kufika katika kituo hicho ili kujifungua kwa njia iliyo salama.
Vijiji vinavyolengwa kunufaika na hospitali hiyo mpya ni pamoja na Sarambei, Lomolo, Banita Kapsitet na sehemu ya Mogotio ambayo iko kwenye mpaka huo.
Hospitali hiyo ilifadhiliwa na shirika la Dandelion Africa kwa ushirikiano na wizara ya afya katika kaunti.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bi Wendo Sahar Aszed alisema kuwa visa vya maambukizi ya magojwa mbalimbali kama vile virusi vya ukimwi pia huripotiwa kwa wingi wakati akina mamahujifungua nyumbani.
‘Waoga’
Alipuuzilia mbali habari ambazo huenezwa vijijini kuhusu akina mama ambao hujifungua hospitalini huku akisema kuwa wao hufanyiwa utani na kudharauliwa mara wengine wakiitwa waoga.
“Usalama wa afya ya mama na mtoto hauwezi kuchukuliwa kama jambo la mzaha. Yafaa sisi sote tuajibike na kueneza habari za kweli kuhusu matibabu kamaili ya hospitalini. Hospitali si mahali pabaya kama vile wengi wenu mnavyodhania,” akasema Bi Wendo wakati akiwahutubia wakazi wa mpakani waliofika kushuhudia uzinduzi huo wa kipekee.
Aliwasihi akina mama ambao wangali katika ujana wao wapuuzilie mbali habari za kupotosha zilizokolea vijijini kuhusiana na matibabu ya hospitalini.
“Kunazo pia mbinu mbalimbali za kisasa za kupanga uzazi zinazotolewa kwenye hospitali bila malipo,” akaongeza.
Alitaja barabara mbovu, siasa duni, utepetevu wa wakazi kukosa kufika kwenye vituo vya afya kwa wakati, kuenea kwa habari potofu vijijini, ushawishi wa itikadi kali za kijamii kama baadhi ya changamoto ambazo huchangia vifo wakati wa kujifua kwa akina mama.