Michezo

Pigo jingine kwa riadha ya Kenya mkimbiaji Kirwa akipatikana na hatia ya kujisisimua kwa kutumia dawa ya panya

June 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa mbio za kilomita 42 za Singapore mwaka 2016, Felix Kirwa ni mwanariadha wa hivi punde kutoka Kenya kupigwa marufuku kwa utumiaji wa dawa kupata ufanisi michezoni.

Kirwa, ambaye alimaliza Eindhoven Marathon katika nafasi ya pili nchini Uholanzi mwaka 2017, amepatikana na hatia ya kutumia dawa iliyopigwa marufuku ya Strychnine.

Mkimbiaji huyu, ambaye alimaliza Singapore Marathon katika nafasi ya pili mwaka 2018 inayotuzwa Sh2,540,750, amepigwa marufuku miezi tisa. Marufuku itakamilika Novemba 14, 2019. Kirwa alisema dawa hiyo iliingia katika mwili wake kwa sababu alikuwa akitumia dawa za kienyeji. Shirika la Kudumisha Uadilifu katika Riadha (AIU) lilisema kwamba kiwango cha Strychnine katika kipimo chake hakikuhitilafiana na malezo yake. Strychnine inapatikana katika orodha ya dawa zilizopigwa marufuku na Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya duniani (WADA) kwa sababu inasisimua misuli.

Kirwa anaingia katika orodha ya karibu Wakenya 60 wakiwemo Rita Jeptoo (marathon), Jemimah Sumgong (marathon), Sarah Chepchirchir (marathon), Kipyegon Bett (mita 800), Agatha Jeruto (mbio za kati), Emily Chebet (mbio ndefu/mbio za nyika) na Cyrus Rutto (mbio ndefu), walionaswa wakitumia dawa haramu kujinufaisha mashindanoni tangu mwaka 2012.

Strychnine ni nini?

Ni ungaunga mkali, mweupe na usio na harufu unaoweza kuingia mwilini kupitia kinywa, kuvutwa kwa pumzi ama kuchanganywa na maji na kudungwa kwenye vena kwa sindano.

Ni sumu ilio na nguvu sana. Inasemekana kwamba kiasi kidogo cha ungaunga huu husababishia mtu madhara makubwa ya kiafya ikiwemo kifo.

Kulingana na tovuti ya kituo cha udhibiti wa magonjwa na kinga (CDC), strychnine inapatikana katika mmea unaojulikana kama Strychnos nux-vomica.

Mmea huu unapatikana sana Bara Asia hasa katika mataifa ya India, Sri Lanka, Indonesia na Ufilipino.

Miaka iliyoenda, strychnine ilipatikana kama vidonge na kutumika kutibu magonjwa mengi ya binadamu. Wakati huu, strychnine inatumika sana kama dawa, hasa ya kuua panya.

Tovuti hiyo inasema kwamba watumiaji wa dawa za kulevya wakati mwingine huchanganya strychnine na Heroin na Kokain.

Dawa hii inaweza kuingia mwilini pia kupitia kwa maji ama chakula kilichotiwa strychnine. Ungaunga huo pia unaweza kuingia mwilini kupitia pua, macho ama kinywa. Dawa hiyo inaweza pia kuvutwa kama sigara ama kutiwa puani.